.

.

.

.

Saturday, November 08, 2008

WAWILI WAJIDHAMINI KWA MILLIONI 800/-(EPA)

Wakati washtakiwa 15 wa wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wakiendelea kusota rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, akiwemo Jeetu Patel, washtakiwa wawili kati yao wamejidhamini kwa Sh. milioni 400 taslim kila mmoja. Pia washtakiwa hao wametimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika kama ilivyoagizwa na Mahakama ya Mkazi Kisutu jijini Dar es Saam. Washtakiwa hao ni Davies Kamungu na Godfrey Mosha wanaokabiliwa na mashitaka 15 ya kugushi, kuwasilisha nyaraka bandia na kujipatia kwa njia ya wizi jumla ya Sh. 2,041,899,876.45. Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Jumatano wiki hii na kusomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Warialwande Lema. Baada ya kusomewa mashitaka yao, upande wa mashitaka ulidai kuwa hauna pingamizi dhidi ya dhamana kwa washitakiwa. Mahakama iliwataka washtakiwa hao kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, ambao watasaini hati ya dhamana ya Sh. milioni 240. Sharti lingine walilopewa na mahakama ni kutoa nusu ya fedha wanazodaiwa kuiba, ambapo ziligawanywa kwa washtakiwa watano. Katika mgawanyo huo kila mshtakiwa alitakiwa kutoa Sh. milioni 400. Pia washtakiwa hao walitakiwa watoe hati za kusafiria na wasitoke nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila idhini ya mahakama. Mahakama pia iliwataka washtakiwa hao kuripoti Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi. Washtakiwa hao wawili waliweza kutimiza masharti ya kutoa Sh. milioni 400 taslim na wadhamini wa kuaminika kama mahakama ilivyotaka.

No comments:

Post a Comment