.

.

.

.

Tuesday, June 16, 2009

NGOMA YA AMATUS LIYUMBA YAZIDI KUWA NGUMU


KIGOGO wa zamani wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba, sasa atalazimika kujipanga upya ili atoke nje kwa dhamana baada ya Mahakama Kuu kufuta masharti yaliyoonekana rahisi ya dhamana yaliyotolewa na Mahakama ya Kisutu.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilimtaka Liyumba, ambaye alikuwa mkurugenzi wa utawala na utumishi kuweka dhamana ya fedha taslimu au hati za mali zenye thamani ya Sh300 milioni katika kesi inayomkabili ya matumizi mabaya ya madaraka katika mradi wa majengo minara pacha ya BoT na kuisababishia serikali hasara ya Sh221 bilioni.
Lakini jana, Mahakama Kuu ilifuta masharti hayo ya dhamana na sasa inamtaka Liyumba aweke fedha taslimu Sh110 bilioni kama dhamana au hati za mali zenye thamani hiyo ili aweze kuwa nje wakati kesi yake ikiendelea.
Kiwango hicho ni nusu ya fedha ambazo Liyumba anatuhumiwa kuiingizia serikali hasara wakati akiwa mkurugenzi wa utawala na utumishi wa benki hiyo.
Akitoa uamuzi huo jana, Jaji Geofrey Shaidi alisema Hakimu Mkazi wa Kisutu, Nyigulila Mwaseba alitafsiri vibaya kifungu cha 148 (5) (e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kwa hoja kwamba kinahusika na makosa ya kuiba na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, lakini sio kusababisha hasara.
“Napendekeza Mahakama ya Kisutu kumpa dhamana Liyumba kwa kuzingatia kifungu cha 148 (5) (e) na utekelezwaji wake ufanywe na hakimu mwingine na sio Hakimu Mwaseba ambaye alitafsiri vibaya kifungu hiki,” alisema Jaji Shaidi.
Jaji Shaidi alisema kifungu hicho ni halali kwani lugha iliyotumika iko wazi na haina utata, hivyo hakubaliani na hoja za upande wa utetezi kwani angefanya hivyo angetafsiri vibaya kifungu hicho.
“Kifungu hiki hakijataja kosa lolote kama wizi au hasara, lakini ili mradi mtu ameshtakiwa na kosa ambalo linahusisha fedha zinazozidi Sh10 milioni, masharti ya kifungu hiki yatatumika,” alisema Jaji Shaidi.
Awali, upande wa utetezi ulijenga hoja kwenye Mahakama ya Kisutu kuwa kifungu hicho kinahusu makosa ya wizi wa fedha tu na hivyo mteja wao apewe masharti mengine, hoja ambayo Hakimu Mwaseba aliikubali na kumtaka Liyumba kuweka dhamana ya thamani ya Sh300 milioni.
Uamuzi huo wa Mwaseba ulifanya Liyumba na mawakili wake kueleza kuwa wangewasilisha hati hizo alasiri ya siku hiyo. Hata hivyo, upande wa mashtaka ulidai kuwa haungekuwa tayari hadi mwanzoni mwa wili iliyofuata.
Lakini badala yake, upande wa mashtaka ulikata rufaa Mahakama Kuu kuiomba kupitia upya masharti hayo.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa, Liyumba alizidisha kiwango kilichokadiriwa katika ujenzi wa majengo ya minara pacha ya BoT na kusababisha serikali kupata hasara ya fedha halisi.
Hata hivyo, mawakili wa Liyumba walidai upande wa mashtaka ulitafsiri kifungu hicho kwa kuungaunga maneno kwani hati ya mashtaka haijaeleza kama pesa hizo ziliingia mfukoni mwa Liyumba licha ya kuelezwa kusababisha hasara.
Hii ni mara ya pili kwa Liyumba kugonga mwamba Mahakama Kuu katika masuala ya dhamana.
Awali, wakati aliposhtakiwa pamoja na aliyekuwa meneja miradi wa BoT, Deogratias Kweka, Liyumba aliwahi kuomba Mahakama Kuu kupitia uamuzi wa masharti ya dhamana uliotolewa na Hakimu Mkazi, Hadija Msongo wa Mahakama ya Kisutu.
Katika masharti hayo, Liyumba na Kweka walitakiwa kutoa Sh55 bilioni kila mmoja, ikiwa ni nusu ya nusu ya kiwango wanachotuhumiwa kuisababishia serikali hasara. Lakini Jaji Projest Rugazia alitupilia mbali hoja hizo na kuagiza kufuatwa kwa uamuzi wa Mahakama ya Kisutu wa kuwataka washtakiwa hao kutoa dhamana ya thamani ya Sh55 bilioni kila mmoja.
Februari 17 Liyumba aliachiwa huru kwa dhamana baada ya mahakama kuridhika na hati ya nyumba yenye thamani ya Sh882 kati ya hati 11 alizowasilisha. Siku moja baada ya kuachiwa, mahakama hiyo ilitoa hati ya kukamatwa tena baada ya kubaini kuwa hati nyingine 10 zilikuwa na mapungufu, ikiwemo hati ya kusafiria ambayo iliisha muda.
Februari 24, Liyumba alifutiwa dhamana na siku iliyofuata mawakili wake waliwasilisha maombi mahakamani wakidai kuwa, hati ya mashtaka ilikuwa na makosa ya kisheria na kutaka wateja wao kuachiwa huru.
Machi 13, Hakimu Msongo aliamua kujitoa katika kesi hiyo baada ya mahakama kulaumiwa kuwa dhamana ya Liyumba ilikuwa na utata na Mei 27, Liyumba na Kweka waliachiwa huru na Hakimu Mkazi Wariyalwande Lema baada ya mahakama kubaini kuwa hati ya mashtaka ilikuwa na makosa ya kisheria na Mei 28 Liyumba alishtakiwa peke yake.
Wakati huo huo, Tausi Ally anaripoti kuwa kesi hiyo ilitajwa jana kwenye Mahakama ya Kisutu na kuahirishwa na Hakimu Mwaseba hadi Juni 29.

No comments:

Post a Comment