.

.

.

.

Saturday, December 19, 2009

AJALI NYINGINE MBAYA SANA


WATU zaidi ya 30 wanahofiwa kufa katika ajali nyingine mbaya iliyohusisha basi la kampuni ya Mohamed Trans ambalo liligongana uso kwa uso na basi dogo aina ya Asia Combi lililotokea eneo la Kandoto, nje kidogo ya mji wa Same mkoani Kilimanjaro.
Basi hilo lenye namba za usajili T 810 AQM na ambalo lilikuwa likitokea Nairobi kwenda Dar es salaam, lililigonga basi hilo dogo ambalo inasemekana lilibeba ndugu waliokuwa wakienda Marangu kwenye harusi.
Hii ni mara ya tatu katika kipindi cha miaka mitatu kwa mabasi ya kampuni ya Mohamed Trans kupata ajali mbaya iliyochukua maisha ya watu wengi, baada ya ajali iliyochukua uhai wa watu 30 mwezi Juni mwaka 2007, na ile ya Julai mwaka huu iliyotokea Korogwe, Tanga na kuchukua roho za watu 25.
Hadi saa 1:00 usiku idadi ya abiria waliothibitishwa kufariki dunia ilikuwa watu 19 na karibu wote ni wale waliokuwa kwenye basi dogo aina ya Asia Combi lenye namba za usajili T 845 BCD lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Moshi.
Mganga mkuu wa hospitali ya Wilaya ya Same, Dk Charles Kifunda aliithibitishia Mwananchi kuwa hadi saa 1: 00 usiku abiria 19 walikuwa wamethibitishwa kufariki ingawa taarifa nyingine zilidai kulikuwa na maiti 28 chumba cha maiti. Hata hivyo alisema kwa wakati huo haikuwa rahisi kutambua waliopoteza maisha.
Basi la Asia Combi linafanya safari za daladala kati ya Sinza na Tandika jijini Dar es Salaam.
Ajali hiyo ilitokea saa 10:00 jioni katika eneo la Kandoto nje kidogo ya mji wa Same mkoani Kilimanjaro katika barabara kuu ya Moshi-Dar es Salaam, eneo ambalo si hatari kwa ajali kama ilivyo maeneo mengine.
Hali ilikuwa ya kutisha kwenye eneo la ajali kutokana na viungo vya watu, ikiwa ni pamoja na vichwa, miguu, mikono na ubongo kuzagaa pamoja na damu nyingi huku kukiwa na vilio kutoka kwa abiria waliojeruhiwa na wananchi ambao walikuwa wakishuhudia maiti na majeruhi hao.
Baadhi ya majeruhi waliokuwa katika basi la Mohamed Trans waliiambia Mwananchi kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa gurudumu la mbele la upande wa kulia, jambo ambalo linatia shaka kuhusu ubora wa matairi yanayotumiwa na kampuni hiyo kutokana na tatizo kama hilo kusababisha ajali ya Korogwe mwezi Julai.
Mmoja wa watu walionusurika katika ajali hiyo, Richard Permena, mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam ambaye alikuwa kwenye basi la Mohamed Trans alisema basi hilo halikuwa kwenye mwendo wa kasi.
"Tulipofika eneo la Kandoto nilisikia kishindo cha kupasuka kwa gurudumu na ndio basi letu likagongana uso kwa uso na lile la Asia Combi na baada ya hapo nilipoteza fahamu sikufahamu nini kiliendelea hadi nilipofika hospitalini," alisema Permena.
Majeruhi mwingine mwenye asili ya kiasia aliyekuwa akitokea Nairobi kwenda jijini Dar es Salaam, Badrudin Pathan alisema hakumbuki nini kilitokea ila amepoteza kila kitu na mkewe yu mahututi.
"Mke wangu anaitwa Hawa amepasuka kichwa yuko ICU (chumba cha wagonjwa mahututi) sijui hali yake ikoje... namshukuru Mungu lakini namuomba amsaidie mke wangu apone," alisema majeruhi huyo.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Ibrahim Marwa aliyekuwa eneo la ajali, alisema watu 11 walikufa papo hapo na wengine waliendelea kufariki wakiwa njiani kupelekwa hospitali ya Wilaya ya Same.
Basi aina ya Asia Combi liliharibika vibaya kiasi cha kumfanya mtu asiamini kama kuna abiria anayeweza kupona.
Ajali ya Korogwe ilisababisha mzozo mkubwa baada ya polisi kumshtaki dereva wa basi hilo kwa makosa ya uzembe, lakini madereva wakatangaza mgomo wakisema kuwa haikuwa kosa lake kwa kuwa ajali ilitokana na tairi kupasuka.
Hata hivyo, Chama cha Wasafirishaji Abiria cha Kilimanjaro na Arusha (Akiboa) kilitaka uchunguzi wa kina ufanyike ili kujua kama basi hilo lilifika eneo la Korogwe katika muda muafaka kama lilivyopangiwa.

No comments:

Post a Comment