Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu Dk. Lawrence Gama, aliyefariki dunia juzi, jijini Dar es Salaam.
“Nimeshtushwa na kuhuzunishwa sana na habari za kifo cha Mzee Lawrence Gama, Mtanzania mwenzetu aliyepata kuwa mtumishi hodari wa umma na mwakilishi mwenye uwezo mkubwa wa wananchi wa Jimbo la Songea Mjini, kilichotokea jana Hospitali ya Aga Khan mjini Dar es Salaam,” alisema.
Alisema Dk. Gama alikuwa kiongozi mfano wa uaminifu na uadilifu katika nafasi zote ambazo alipata kuzishikilia maishani mwake.
“Iwe katika utumishi wa Serikali ambako alipata kuwa Mkuu wa Mkoa, iwe utumishi wa Jeshi ambako alipata kuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT), iwe utumishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambako alipata kuwa Katibu Mkuu, ama kwenye nafasi ya uwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Songea Mjini ambako alipata kuwa Mbunge, Mzee Gama alikuwa mfano wa uongozi bora, na taifa letu litakosa sana busara zake na mchango wake mkubwa katika jitihada za kujitafutia maendeleo,” alisema.
Rais Kikwete alisema kwa wakati huu wa msiba, mawazo yake yako kwa familia ya Mzee Gama ambayo imepotelewa na babu, baba, mzazi, mlezi na kiongozi wa kuaminika.
Wakati huohuo, mwili wa Dk. Gama unatarajiwa kuagwa leo jijini Dar es Salaam baada ya misa itakayofanyika Kanisa Katholiki la Mtakatifu Gasper, Mbezi jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment