.

.

.

.

Sunday, August 14, 2011

BALOZI GEORGE NH'IGULA AFARIKI DUNIA

Tanzania 50 Plus Campaign imepata msiba mkubwa kufiwa na mwanaharakati wa kutoa Elimu, Utetezi na Msaada juu ya saratani ya tezi dume – prostate cancer. Taarifa ya msiba huu imepatikana mapema asubuhi toka kwa mtoto wake Paul. Umauti huo ulimpata wakati akitibiwa katika hospitali ya Mikumi hapo Magomeni.

Katika uhai wake Hayati Balozi Nhigula amekuwa mwalimu na baadaye kuwa mwanadiplomasia mwandamizi akiwakilisha nchi yetu nchi mbali mbali zikiwemo Uingereza, Misri, Marekani na Japani.

Baada ya kustaafu alirudi nchini na kuendelea na majukumu mbalimbali ikiwemo ubunge wa Kwimba kwa miaka kumi hadi mwisho wa awamu ya Rais Mkapa. Wakati huo huo alikuwa mwenyekiti wa Japan-Tanzania Friendship Association.

Hayati Balozi Nhigula mwanzoni mwa mwaka jana huku akisumbuliwa na saratani ya tezi dume – prostate cancer kwa muda, alipata bahati ya kusoma makala kuhusu gonjwa hilo katika gazeti moja. Akachukua jukumu kufuatilia chanzo cha andiko hilo ndipo alipofika ofisi za Tanzania 50 Plus Campaign ambako alipatiwa ushauri nasaha na baadaye kupata tiba. Baada ya tiba alijiunga na kampeini na alikuwa mtu muhimu na mstari wa mbele katika kampeini hii. Kwa kifupi alikuwa kamanda wa kutegemewa!

Tunaomba uungane na Tanzania 50 Plus Campaign katika msiba huu mkubwa. Maiti ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo. Msiba upo Tabata magorofa ya Bima. Marehemu ameacha mjane na watoto watano – wanaume wane na wakike mmoja. Kwa maelezo zaidi wasiliana na mtoto wake Paul Simu: 0757676454.

SISI TULIMPENDA ILA BWANA AMEMPENDA ZAIDI.

JINA LA BWANA LISIFIWE !

No comments:

Post a Comment