Ziara ya mafunzo ya washiriki wa shindano la Vodacom Miss Tanzania 2011 imeendelea Mikoa ya kanda ya Kaskazini na warembo hao wamepata fursa ya kutembelea kaburi la aliyewahi kuwa Waziri Mkuu Hayati Edward Moringe Sokoine.
Wakiwa eneo la Monduli warembo hao walipokelewa na Mtoto wa Sokoine Namelok Sokoine ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM) mkoa wa Arusha.
Mbunge huyo alipata fursa ya kuwapa historia fupi ya maisha ya baba yake hasa alipokuwa Waziri Mkuu,mapema walipowasili wilaya ya monduli walipokelewa na mke wa Waziri Mkuu mstaafu Mama Regina Lowasa na viongozi wengine wa wilaya hiyo,Katika hafla hiyo mgeni rasmi alikuwa ni Mbunge wa Viti Maalum wa mkoa wa Arusha Namelok Sokoine na alipata fursa ya kuwaasa warembo hao pamoja na ziara yao ya kutembelea vivutio vya utalii na maeneo ya kihistoria watumie fursa hiyo kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike hasa jamii ya kimasai,alisema jamii ya kimasai ambayo inajishughulisha na ufugaji haijatoa kipaumbele katika kumsomesha motto wa kike hivyo ziara ya warembo hao inaweza kutumika kubadilisha mtizamo huo.
Akizungumzia ziara hiyo Meneja Uhusiano na Habari kwa Njia ya Mtandao wa Vodacom Tanzania Matina Nkurlu alisema washiriki hao walijifunza vitu mbalimbali alivyovifanya Hayati Sokoine enzi za uhai wake.
Mara baada ya kutoka katika eneo hilo warembo hao 30 pia walitembelea shule ya Maasai Girls iliyopo Monduli kabla ya kupata chakula cha jioni.
“Ziara yetu bado inaendelea na warembo wanaendelea kujifunza kupitia elimu inayotolewa na wataalam mbalimbali wanaopata fursa ya kukutana na warembo wetu. Ni matumaini yetu wataitumia elimu hii kulitangaza taifa katika medani za kimataifa,” alisema Nkurlu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Lino Agency ambao ndio waandaaji wa Vodacom Miss Tanzania Hashim Lundenga alisema warembo hao pia watatembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorogoro NCAA, ili kujionea moja ya maajabu saba ya dunia.
Akifafanua Lundenga amesema mwaka huu wanataka warembo wenye sifa ikiwemo elimu, muonekanao na tabia nzuri ili mshindi atakayepatikana aweze kutuwakilisha vema katika medani za kimataifa hususani kujua vivutio vya kitalii vilivyopo nchini.
“Baada ya kutoka Mikumi ziara hii ya mafunzo sasa imeingia kanda ya kaskazini, tukiwa safarini kutokea Morogoro warembo walipata fursa ya kupiga picha katika maeneo mbalimbali ikiwemo daraja la mto wami na mji maarufu wa Moshi mkoani Kilimanjaro,” alisema Lundenga.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wengine mrembo Jennifer Kakolaki alisema kuwa wanaifurahia ziara hiyo kwani mbali ya kujionea rasirimali tofauti zilizopo nchini wanajifunza mengi kuhusiana na utalii wa ndani.
“Kiujumla Watanzania hawana budi kutenga siku maalum katika mwaka ili kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo nchini. Binafsi nimepanua kiwango changu cha ufahamu kuhusiana na utajiri wa rasilimali za taifa zilizopo nchini,” alisema Jennifer.
Mwaka huu warembo hao wameingia kambini kwa mfumo tofauti na uliozoeleka kwani wamewekwa kwenye jumba maalum la ‘Vodacom House’ ambapo matukio yao yatakuwa yakioneshwa kupitia Startv na Clouds TV na watazamaji watapata fursa ya kupiga kura kuchagua mrembo watakayemuona anafaa.
No comments:
Post a Comment