.

.

.

.

Wednesday, August 17, 2011

MOTO MOTO BUNGENI DODOMA

LICHA ya kupata wakati mgumu Bungeni, Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imepitishwa jana huku Waziri wake, Profesa Anna Tibaijuka akitoa onyo kwa wanaohodhi ardhi kwa muda mrefu bila kuiendeleza akisema: “Fungate yao imekwisha.”

Kauli hiyo ya Profesa Tibaijuka imekuja siku moja baada ya kambi ya upinzani bungeni kupitia Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee kutaja orodha ndefu ya vigogo hao wa CCM wakiwamo Marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Mawaziri Wakuu wastaafu, John Malecela na Frederick Sumaye.

Wengine waliotajwa ni Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Philip Mangula na aliyekuwa Naibu wake (Bara), Hassan Ngwilizi akisema kwamba wamehodhi ardhi kubwa mkoani Morogoro bila kuiendeleza. Hata hivyo, alisema ni Mkapa pekee aliyeendeleza eneo lake.

Mwingine aliyetajwa na Mdee ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Nawab Mulla.Akijibu hoja hiyo na nyingine bungeni jana Profesa Tibaijuka, kwa kifupi alisema kwa wamiliki wote wa ardhi ambayo haijaendelezwa: “Honeymoon is over” (fungate imekwisha) na kwamba wizara yake itapitia miliki za mashamba na maeneo mengine yasiyoendelezwa kisha kuchukua hatua stahili.

“Wizara yangu itafanyia ukaguzi maeneo haya ya ardhi, hivyo wanaomiliki mashamba ambayo bado hayajaendelezwa basi wajue kwamba “honeymoon is over."


Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema) katika hoja hiyo, alisema vigogo hao wanahodhi maeneo makubwa ya ardhi huku wananchi hasa wale waishio jirani nayo wakikosa ardhi hali ambayo aliita ni hatari kwa amani ya nchi.

Bila kuwataja kwa majina vigogo hao kwa majina kama alivyofanya waziri kivuli, Profesa Tibaijuka pia alisema kwamba hata wale ambao wamemilikishwa ardhi na kuamua kuikodisha kwa wananchi na kuwatoza kodi, watashughulikiwa.

No comments:

Post a Comment