.

.

.

.

Monday, December 19, 2011

MAALIM SEIF AFURAHISHWA NA SELIKALI YA MSETO

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema anaridhishwa na mafanikio ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. 

Amesema kutokana na hali hiyo, hafikirii kwamba Zanzibar inapaswa kurejea katika mfumo tenganishi ambao ulisababisha mgawanyiko mkubwa visiwani. 

Maalim Seif aliyasema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi kuzungumzia mafanikio na changamoto za mwaka mmoja wa Serikali hiyo inayoundwa na vyama vya CCM na CUF. 

“Naam, ninaridhika sana na mafanikio yaliyopatikana katika Serikali hii, sio mafanikio madogo, ni ya kuridhisha,” alisema Seif na kuongeza kuwa kila jambo lina changamoto zake. 

Alisema kutokana na hilo, changamoto zilizopo hazina budi kurekebishwa ili kuiwezesha Serikali hiyo iliyoundwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, kupata mafanikio makubwa zaidi. 

Alisema ukilinganisha na Serikali kama hizo zilizopo Zimbabwe na Kenya, ya Zanzibar imeonesha kwenda vizuri licha ya kuwepo kwa upungufu kadhaa. 

Alisema katika kuendesha Serikali hiyo wanatumia sera za chama anachotoka Rais, lakini kwa busara za Rais Dk. Ali Mohammed Shein, Serikali hiyo inatekeleza sera zote zenye manufaa wa ustawi wa Zanzibar hata kama zinatoka kwa chama kingine. 

Alisema licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza katika mwaka mmoja wa Serikali hiyo, yapo mafanikio katika uboreshaji wa kilimo katika mazao ya chakula na biashara, kuimarisha sekta ya uvuvi, kuboresha hali za maisha za wafanyakazi na kukuza teknolojia ya Habari na Mawasiliano. 

Katika kilimo, alisema zao la karafuu limepanda ambapo mwaka huu, kilo moja inanunuliwa kwa Sh 15,000, na inatarajiwa kuwa ifikapo Mei mwakani, kwa kisiwa cha Pemba pekee, wakulima watapata Sh bilioni 50 kutokana na mauzo ya karafuu. 

Katika uvuvi, Maalim Seif alisema Serikali imechukua hatua kuifanya rasilimali ya bahari kuwanufaisha wananchi, na hivi sasa wawekezaji wengi wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta hiyo. 

“Katika kuendeleza sekta ya uvuvi, tayari Serikali imewapeleka wananchi 30 huko China kujifunza mbinu za kufuga samaki,” alieleza Maalim Seif. 

Maalim Seif alisema mbali ya mafanikio hayo, zipo changamoto kadhaa zikiwemo za baadhi ya watendaji wa Serikali kutofahamu malengo ya kuanzishwa kwa mfumo wa Serikali shirikishi, badala yake kuendelea na mfumo tenganishi. 

“Badala yake wanaendesha shughuli za umma kwa taratibu zile zile ambazo hazisaidii sana kuimarisha umoja wetu,” alieleza Seif na kuongeza kuwa baadhi ya watendaji hao wanafanya kazi kwa mazoea. 

Alisema pia yapo malalamiko mengi kuhusu suala la ardhi, ambayo hata hivyo, alibainisha kuwa Serikali inayafanyia kazi na tayari inapitia upya sera ya ardhi na sheria zote zinazohusu masuala ya ardhi. 

“Kuna malalamiko makubwa ya kuwa wanafunzi wengi hawajafaidika na mikopo ya kuwawezesha kupata elimu ya juu. Hili linatokana na uwezo mdogo wa Serikali,” alisema na kuongeza: “Wanafunzi wanaohitaji mikopo ni zaidi ya 1,500. 

Uwezo uliopo kwa mwaka huu wa fedha ni kuwapatia huduma hii muhimu wanafunzi 191 tu. Serikali itakuwa ikiongeza fungu la mikopo hii kila mwaka ili wanafunzi wanaofaidika waweze kuongezeka kila mwaka.” 

Aidha, alisema baadhi ya wananchi wanalalamikia kuwa wananyimwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, na kuona kuwa hiyo ni haki ya kila mtu na Rais Shein alishatoa maelezo kwamba kila mtu apatiwe, hivyo ofisa asiyetekeleza hivyo, anafanya utovu wa nidhamu. 
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), aliwataka Wazanzibari kushirikiana kwa pamoja kuinua ustawi wa nchi yao.

No comments:

Post a Comment