.

.

.

.

Monday, January 09, 2012

JK INTERNATIONAL YAKUMBWA NA KASHFA

UWANJA wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere umekumbwa na kashfa nyingine, baada ya abiria, Mtanzania aliyekuwa tayari amegongewa muhuri wa uhamiaji kwenye hati yake ya kusafiria kwenda nje ya nchi, kutokomea kusikojulikana akiwa amewatapeli raia wa Poland, dhahabu na fedha vyenye thamani inayokadiriwa kufikia Sh80 milioni.

Tukio hilo limetokea huku kukiwa na kumbukumbu ya tukio la Desemba 2, mwaka jana pale abiria Zainabu Kaswaka alipokutwa na bastola kwenye ndege ya shirika la Emirates wakati akisafiri kwenda nchini Uingereza.

Wiki mbili baadaye, Desemba 17 mwaka jana, vyanzo vya habari za kiuchunguzi vimethibitisha kwamba raia wawili wa nchini Poland, Hery Jabloiw  ambaye kitaaluma ni mhandisi na mwingine ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, walitapeliwa walipokuwa katika harakati za kusafiri kuelekea Warsaw kwa ndege ya saa 5:00 usiku ya Shirika la KLM.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, raia hao wawili wa kigeni, walikuwa nchini ambako siku zote walikuwa na urafiki na raia huyo wa Tanzania (jina tunalihifadhi kwa sasa) ambaye aliwasaidia kununua madhini ya dhahabu kwa mapatano kwamba wangemlipa kiasi fulani cha fedha.

Siku safari walifika naye uwanjani hapo kwa ajili ya kwenda naye Warsaw, Poland ambako wangemlipa malipo ya mwisho kwa mujibu wa makubaliano yao.

Vyanzo hivyo viliongeza kwamba katika mazingira ya kutatanisha, kabla ya kufanyiwa ukaguzi na kuingia uwanjani, raia huyo wa Tanzania aliwaambia Wapoland hao kwamba, madini wasingeweza kusafiri nayo kama mzigo wa mkononi na badala yake aliwashauri ufanyike utaratibu wa kusafirishwa kama kifurushi katika ndege ya mizigo.

Kufuati ushauri huo, Mtanzania huyo alikwenda kushughulikia suala hilo na baadaye kurejea na nyaraka bandia zilizothibitisha kwamba mzigo ulikabidhiwa kwenye ndege kwa ajili ya kusafirishwa.

Baada ya mchakato huo, tapeli huyo na raia hao wa kigeni walipita kwenye mashine za ukaguzi, kisha kwenda ofis za Idara ya Uhamiaji ambako waligongewa mihuri kwenye hati zao za kusafiria.

Taarifa hizo zinadai kuwa wakiwa tayari wamepita idara ya uhamiaji na kupata idhini ya kusafiri kwenda ng’ambo na baadaye kukaa katika chumba cha kusubiria ndege, ghafla Mtanzania huyo aliwaambia Wapoland hao kwamba kama wana fedha za Tanzania wampatie ili akazibadilishe kuwa dola za Marekani.

Katika mazingira ya kushangaza, Mtanzania huyo alitoka nje na fedha hizo Sh100,000, licha ya kwamba alishafanyiwa ukaguzi na kugongewa muhuri wa uhamiaji kwenye hati aya kusafiria.

Mwananchi lilibaini kwamba, raia huyo ambaye tayari alikuwa amelipwa ujira wa Sh1.7 milioni na Wapoland hao kama shukrani ya kuwasaidia katika utafutaji wa madini, alipotoka nje alipita sehemu zote za ukaguzi bila kuulizwa na akatokomea.

Vyanzo hivyo vilisema Wapoland hao walipanda ndege kwa matarajio kwamba rafiki yao angerejea, lakini haikuwa hivyo kwani ndege ilipokaribia kuruka, walitoa taarifa kwa vyombo vya usalama uwanjani hapo, hivyo wakaahirisha safari.

Walikaa usiku mzima uwanjani bila kumwona raia huyo, na hapo walibaini kwamba walikuwa wametapeliwa na hawakuwa na fedha za akiba kwani walimwambia Mtanzania huyo kwamba, kiasi kingine cha fedha za shukrani wangempatia baada ya kufika Warsaw.

"Wale Wapoland walikaa uwanjani pale hadi asubuhi wakawa hawana hata senti moja. Kuna askari mmoja aliwasaidia na kuwapa chai na chapati. Lakini, watu wanahoji iweje mtu aliyegongewa mhuri wa uhamiaji tayari kwa kusafiri, arejee tena nje na aruhusiwe?" kilohoji chanzo kimoja uwanjani hapo na kuongeza:,
"Kwa sababu, kiutaratibu mtu ukishagongewa mhuri wa uhamiaji maana yake tayari unatakiwa usafiri ng'ambo. Kama akipatwa na dharura, lazima aombe wahusika wakamsadie hawezi kutoka hivihivi, hili ni kosa lakini hapa inaonekana kuna mchezo." 

Mkurugenzi 
Alipoulizwa Mkurugenzi Mkuu wa Uwanja huo, Moses Mlaki alisema asingeweza kuongea suala hilo kwenye simu, na badala yake alitaka apewe maswali kwa maandishi.

Mkuu wa usalama wa uwanja huo, aliyejulikana kwa jina la Msangi alipoulizwa yeye alisema asingependa kuzungumzia suala hilo kwani eneo lake la kazi, linaishia kwenye ukaguzi wa mashine tu.

Baadhi ya vyanzo vyetu kinachochangia uhalifu ni baadhi ya vibanda vinavyotumiwa na askari kulinda uwanja huo kutokuwa na huduma za umeme na maji hali inayowafanya kufanyakazi katika mazingira magumu.
"Yaani hakuna maji, umeme wala nini, angalia tunalinda mitambo nyeti ya uwanja yenye thamani kubwa lakini maeneo yetu ya kazi hayana umeme wala maji. Tutafanyaje kazi katika hali hii?," kilihoji chanzo kimoja.   
  

No comments:

Post a Comment