.

.

.

.

Sunday, April 29, 2012

MAWAZIRI WA JK MATUMBO JOTO

WAKATI mawaziri wanaounda Serikali ya Awamu ya Nne wanaendelea kupata usingizi wa mang’amung’amu kwa hofu ya kupanguliwa, kuna taarifa kwamba idadi kubwa ya mawaziri wa zamani wataachwa na sura mpya hususan vijana kutawala baraza jipya. 

Joto la mabadiliko ya Baraza la Mawaziri limeshika kasi baada ya Kikao cha Kamati Kuu (CC) ya CCM iliyokutana juzi jijini Dar es Salaam juzi na kuridhia mapendekezo ya Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa chama hicho, kuwataka mawaziri wanaoandamwa na kashfa mbalimbali katika wizara zao, kuachia ngazi.

Taarifa ya Rais Kikwete kutaka kusuka upya Baraza la Mawaziri ilitangazwa juzi na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye alipokutana na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumalizikia kwa kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya CCM.  
 
Vyanzo vya gazeti hili vimeeleza kuwa mbali na Rais kutumia kigezo cha udhaifu uliobainishwa kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), atawaengua pia wale wanaoshindwa kuwajibika na wale wenye kasi ndogo ya uongozi.

Mawaziri wanaotuhumiwa kushindwa kuwajibika, wengi wao ni vijana hivyo huenda akachagua vijana wenzao kuchukua nafasi zao. 

Habari hizo zinaeleeza kuna uwezekano mkubwa katika mabadiliko hayo, mawaziri wazee na wagonjwa wakakumbwa na fagio hilo. 

Vijana wanaotajwa kuwa huenda wakaingia katika Baraza jipya la Mawaziri ni pamoja na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba, Mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi, Mbunge wa Handeni, Dk Abdallah Kigoda, Mbunge Kahama, James Lembeli, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango na Mbunge wa Igunga Dk Dalaly Peter Kafumu

No comments:

Post a Comment