.

.

.

.

Thursday, May 03, 2012

VIGOGO KUPOTEZA MAHEKALU YAO YA UFUKWENI


WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ametoa wiki mbili kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, kutoa notisi kwa watu waliojenga ndani ya meta 60 pembeni mwa bahari na maeneo oevu, kuonesha hatimiliki zao.

Katika agizo hilo, amesema ikiwa watakuwa na hatimiliki halali, Serikali itajadiliana nao na wakikutwa bila hatimiliki, watanyang’anywa maeneo yao bila fidia.

Alisema hayo juzi alipofanya ziara katika Manispaa ya Kinondoni kwenye maeneo yenye malalamiko ya upangaji, upimaji na uendelezaji na kuagiza kubomolewa kwa baadhi ya majengo baada ya kukutwa yamejenga ndani ya barabara.

Aidha, aliziagiza halmashauri zote nchini, kuondoa majengo yaliyojengwa kinyume cha sheria na kuhakikisha wanasimamia upangaji na uendelezaji miji, kama ilivyoainishwa katika sheria za nchi ya Mipangomiji ya mwaka 2007.

“Maendelezo yote hapa ni batili, tunataka maeneo yote yaliyo ndani ya meta 60 yaondolewe bila ubaguzi, kwa sababu hakuna mtu aliye juu ya sheria.

“Kama wana hati, tutazungumza ila kama hawana, wataondoka mikono mitupu, hizi fukwe lazima tuzifunge kwa maslahi ya vizazi vyetu,” alisema.

Alisema kuwa uendelezaji na utumiaji wa ardhi ndani ya miji unatakiwa kuzingatia mpango uliopo ili kuleta uwiano mzuri wa maendelezo jirani au katika jamii na hivyo kuondoa mgongano wa matumizi ya ardhi.

“Limekuwapo tatizo kubwa la miji yetu kuendelezwa kiholela kana kwamba hakuna sheria yoyote inayosimamia uendelezaji wa miji. Hali hii inachangia kuwepo kwa kero kwa jamii na uharibifu wa mazingira na hili limekuwa tatizo sugu katika miji yetu,” alisema.

Alisema operesheni hiyo na ukaguzi wa maeneo ambayo hayajafuata utaratibu ni ya nchi nzima, ila ameamua kuanzia ziara yake Kinondoni kutokana na kwamba amekuwa akipokea simu si chini ya 50 kila siku za malalamiko ya uvunjwaji wa sheria ya mipangomiji katika manispaa hiyo.

“Mipangomiji haifanyi kazi kwa sababu sheria mnazozisimamia hamzifahamu, kuna siku tutawanyang’anya madaraka na tutakuwa tunapanga kila kitu wizarani… sasa hivi ni wakati wa vitendo, lazima tufanye kazi Watanzania waelewe na waone,” alisema.

Alisema kutokana na ujenzi holela, yapo maeneo ambayo kipindi cha mvua mafuriko yanazidi, kwa kuwa mikondo ya kupitisha maji imebadilishwa matumizi na watu wachache kujimilikisha na kujenga nyumba bila vibali.

Katika ziara yake hiyo Mbezi-Kawe aliagiza eneo la kwa Msomali kiwanja namba 1057 karibu na kiwanja namba 944 ambalo limejengwa ghorofa livunjwe kwa kuwa mwendelezaji wa eneo hilo amejenga ndani ya meta 10 za barabara.

Alisema wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakilalamika kuwa hawana barabara ya kuingilia, hivyo lazima haki itendeke bila kuangalia uwezo wa mtu.

Aliagiza viwanja namba 2020 na 2021 vya Kawe Beach; viachwe wazi kwani ni sehemu ya kupumulia bahari, na wahusika wapewe hati ya kusimamisha ujenzi haraka.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alipongeza jitihada za Wizara hiyo na kutaka hatua stahiki zichukuliwe kwa maslahi ya Taifa.

 

No comments:

Post a Comment