Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2011; imeendelea kufichua namna kundi la watumishi wa umma na wafanyabiashara wakubwa wanavyoitafuna Tanzania. Utouh aliwasilisha taarifa hiyo bungeni mwishoni mwa wiki. Fedha na mali za umma zenye thamani ya mabilioni ya shilingi, ama zinaibwa au zinachukuliwa kwa namna ambayo ni vigumu kuamini kama kweli viongozi wakuu wa kitaifa wana dhamira ya kutokomeza ufisadi uliovuka mipaka.
Kuuzwa kwa viwanja, majengo ya Serikali
CAG amebaini kuwa kiwanja kilichopo katika Kitalu Na. 10 katika Barabara ya Nyerere, kimeuzwa kwa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) kinyemela. Amesema wakati uuzaji kiwanja hicho ulipaswa uratibiwe na Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC - mrithi wa PSRC), kazi hiyo ilifanywa na watu wasiokuwa na mamlaka kisheria.
Nyaraka za mawasiliano kati ya MeTL, Wizara ya Fedha na Msajili wa Hazina zinazohusiana na uuzaji kiwanja hicho, zinaonyesha kuwa Wizara ya Fedha na Msajili wa Hazina ndiyo waliojihusisha moja kwa moja katika uuzaji wa mali hiyo ya umma, kwa kutoa maelekezo kwenye menejimenti ya CHC. Bodi ya Wakurugenzi haikushirikishwa kabisa.
Hatimaye kiwanja hicho kiliuzwa kwa MeTL kwa Sh bilioni 2.046 bila kufuatwa kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2005.
Katibu wa Waziri aamuru kampuni ilipwe Sh bilioni 2.34
Utata wa matumizi mabaya ya fedha za umma, umemkumba aliyekuwa Katibu wa Waziri mwenye dhamana ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji kuhusu kiwanja namba 192 kilichopo Barabara ya Nyerere. Alimwandikia barua Mwenyekiti wa PSRC ailipe kampuni ya DRTC Sh milioni 954.72.
Hata hivyo, Meneja Mkuu wa DRTC akamwandikia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC akitaka alipwe haraka kiasi cha Sh bilioni 2.349. Kwenye barua hiyo, Meneja wa DRTC alisisitiza kuwa malipo hayo ni maelekezo kutoka serikalini, licha ya ukweli kwamba yalikuwa ni makubwa kuliko madai halisi na akalipwa.
Kuuzwa kwa jengo la kampuni ya umma ya TMSC
Jengo la kampuni ya Tanzania Motors Services (TMSC) lipo katika kitalu namba 24 katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam. Jengo hilo liliuzwa kwa kwa kampuni ya Saddiq Super Service Station (SSSS) kwa Sh bilioni 1.3. Kampuni hiyo ilitoa malipo ya awali ya asilimia 10, yaani Sh milioni 130. Baadaye Wizara ya Fedha ikaitaarifu CHC kuwa Serikali imeghairi kuliuza jengo hilo lililopo kitalu namba 24 kwa kampuni ya SSSS. Wizara ya Fedha ikaitaka CHC ikubaliane na SSSS kuwafidia, kwani tayari kampuni hiyo ilishatoa kianzio cha Sh milioni 130.
Kuona hivyo, kampuni ya SSSS ikawasilisha madai ya kulipwa fidia ya Sh bilioni 3.894 kwa ajili ya kupoteza biashara yake na Sh milioni 500 kama fidia kwa usumbufu. Hatimaye ikaamuliwa kuwa SSSS ilipwe Sh milioni 964 ambamo ndani yake kulikuwa na Sh milioni 130 ilizotoa awali na gharama za usumbufu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha alikuwa Mwenyekiti wa kikao kilichoidhinisha malipo hayo. Akawasilisha katika Wizara ya Fedha ambayo yeye ni kiongozi, ili ilipe kiasi hicho cha fedha kwa maelekezo ya kikao alichokiongoza yeye mwenyewe.
Kwa uamuzi huo, Wizara ya Fedha ikailipa moja kwa moja SSSS Sh milioni 964.2; ilhali kama ni malipo, basi yalipaswa kufanywa na CHC. Malipo hayo, kwa mujibu wa taarifa ya CAG, yanaibua maswali juu ya dhamira ya Wizara ya Fedha kulipa fedha hizo haraka haraka bila kuishirikisha Menejimenti wala Bodi ya Wakurugenzi ya CHC.
Malipo ya kushangaza kwa kampuni ya Tantrack
Tantrack Agencies ilikuwa mpangaji katika jengo la TMSC lilipo kitalu namba 24, Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam. Ilipanga kwa miaka miwili kuanzia Julai Mosi 1993. Kampuni hiyo inasema ilitumia Sh milioni 24 kukarabati jengo kwa wakati wote wa mkataba wake wa upangaji, licha ya ukweli kwamba jambo hilo halikuwamo kwenye mkataba iliyoingia na TMSC. Ikakataa kulipa ada ya pango ikisema fedha hizo zilizotumika kwenye ukarabati zitambuliwe kuwa ndiyo ada ya pango.
Tantrack ikafungua kesi ya madai namba 257 ya mwaka 1995 katika Baraza la Nyumba Mkoa wa Dar es Salaam (DRHT) dhidi ya TMSC, kwa kigezo kwamba TMSC ilikuwa ikivunja makubaliano. Ilifanya hivyo baada ya TMSC kuiandikia barua ikiipa notisi ya miezi sita ihame kutokana na kutotekeleza makubaliano ya mkataba.
Wakati hayo yakiendelea, jengo la TMSC likauzwa kwa njia ya mnada kwa African Terminal Limited (ATL) kwa amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa Sh milioni 3. CHC ikapeleka vielelezo vyake mahakamani ikionyesha mkataba ulivyokuwa kati yake na Tantrack. Kabla rufaa haijasikilizwa, ATL ikaweka pingamizi. Sasa ni miaka 15 suala hilo likiwa halijaamuliwa.
CAG anasema imebainika kuwa kuna uzembe na kutowajibika kwa pande zote mbili zinazopambana kwenye mgogoro huo.
Utata Kitalu namba 33 kilichotwaliwa na Kampuni ya Maungu Seeds
PSRC iliingia makubaliano na kampuni ya Maungu Seeds, kwa ajili ya kununua kiwanda cha Mzizima Maize Mill kilichopo Kitalu namba 33, Barabara ya Saza katika Eneo la Viwanda Chang’ombe jijini Dar es Salaam.
Makubaliano hayo yalitiwa saini Septemba 1, 2004; na gharama ya ununuzi ilikuwa Sh milioni 620. Malipo yalikuwa yafanywe kwa awamu tatu. Maungu ikaanza kulipa Sh milioni 200 na kutoa dhamana ya benki (TIB) ya Sh milioni 420.
Ikakubaliwa kuwa PSRC ingeikabidhi kampuni ya Maungu kiwanda hicho ndani ya miezi mitatu baada ya kutiliana saini ya ununuzi, na kwamba Maungu ingekabidhiwa nyaraka zote baada ya kukamilisha malipo. Iliyokuwa PSRC ikashindwa kukabidhi kiwanda kwa mujibu wa makubaliano kwenye mkataba kutokana na kwamba, kiwanda kilikuwa rehani kwa kampuni ya CDC London ya Uingereza tangu mwaka 1959.
Hatimaye, ilipofika Aprili 26, 2006 rehani ikawa imeondolewa, lakini tayari muda wa dhamana ya benki ulikuwa umekwisha. Kiasi cha Sh milioni 420 kikawa hakijalipwa. Mwaka 2010 kampuni ya Maungu ikafungua kesi ya madai na ikaamuriwa kuwa ipewe hati ya eneo yenye namba 6639. PSRC (CHC) ikaamuriwa iilipe Maungu Sh milioni 200 haraka. Fedha hizo ni zilezile ilizokuwa imetoa kama malipo ya awali na ikarejeshewa.
Kimsingi, Maungu ikawa haijalipa chochote, lakini ikawa imepewa kiwanda cha Mzizima bure kabisa bila kulipa kiasi chochote kwa mali hiyo ya umma.
Madeni ya Simu 2000 yafutwa kienyeji
CAG ameonyesha wasiwasi mkubwa kwa uamuzi wa CHC wa kufuta madeni mengi ya iliyokuwa kampuni ya Simu 2000. Kampuni hiyo iliundwa na kuongozwa na familia ya Mama Anna Mkapa, kwa ajili ya kuuza zilizokuwa mali za Shirika la Posta na Simu. Kuna habari kwamba familia hiyo ilijitwalia mali kadhaa zenye thamani ya mabilioni ya shilingi. Miongoni mwa majengo yaliyouzwa ni maghorofa yaliyopo Ilala.
Ulaji Chuo cha Ubaharia (DMI)
Ukaguzi uliofanywa na CAG umebaini kuwa Sh milioni 83.96 zimelipwa kama takrima na fedha za kujikimu kwa viongozi bila kuidhinishwa na mamlaka za kisheria. Katika malipo hayo, maofisa wa Wizara ya Mawasiliano walilipwa Sh milioni 12; na Sh milioni 51.8 zililipwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la DMI kama posho ya madaraka (honorarium), mafuta na posho ya vikao.
Sh milioni 2.6 zililipwa kwa maofisa wa akaunti wa DMI bila wao wenyewe kuhudhuria vikao; Sh. milioni 10.4 zililipwa kwa watumishi wa DMI kama posho ya kujikimu Juni, 2009 bila wenyewe kuhudhuria kile kilichoitwa kuwa ni kikao cha kikosi kazi cha kupitia mitaala ya DMI.
Katika hatua nyingine, DMI ilipokea Sh milioni 385 kwa ajili ya kuwalipa wadeni wake, lakini ukaguzi umebaini kuwa ni 205.8 pekee zilizotumika. Wafanyakazi 12 wa DMI wamelipwa mishahara ya ngazi ya PGSS 5 na zaidi bila kuidhinishwa na Baraza DMI. Aidha, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala amekuwa akijilipa mshahara kwa kiwango cha PHTS ambacho hakikuidhinishwa.
Kompyuta za msaada zaibwa, zanyofolewa vifaa
Ukaguzi umebaini kuwa Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza, kilitoa msaada wa kompyuta 25 kwa DMI kwa ajili ya maktaba yake. DMI ilimlipa wakala wa utoaji vifaa hivyo bandarini Sh milioni tatu Desemba 7, 2007. Lakini hadi ukaguzi unafanywa, kompyuta hizo zilikuwa hazijawasilishwa kama ilivyotarajiwa.
Baadaye imebainika kuwa kati ya kompyuta hizo, ni kompyuta 13 pekee zilizowasilishwa katika maktaba, na kwamba ni kompyuta nne pekee zinazoweza kukarabatiwa. Kompyuta kenda haziwezi kutengenezwa kutokana na kuibwa vifaa muhimu kama Ram, Processors, Hard disks, Power Supply na Mother Boards.
Bohari ya Dawa (MSD) inaingiza vifaa feki
Pamoja na kuwapo upotevu wa mamilioni ya shilingi zinazotolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, CAG amebaini kuwa baadhi ya vifaa na dawa vinavyosambazwa na MSD havina ubora. Ametoa mfano wa mashine za kupima shinikizo la damu na vifaa vinavyotumika kubebea wagonjwa.
Pia dawa kama kwinini imebainika kuwa inasambazwa nyingine ikiwa na ubora wa hali ya chini, kutokana na pengine kutohifadhiwa vizuri. Aidha, ukaguzi umebaini kuwa vitambaa vinavyotumika kunyonya damu wakati wa upasuaji huwa vipo chini ya kiwango.
Ukaguzi umebaini kuwa Sh bilioni 3.95, dola milioni 9.4 na euro milioni 1.5 ambazo zimetumika bila kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni ya MSD na hivyo kukiuka Sheri ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na Kanuni 41 ya Tangazo la Serikali namba 97.
Aidha, imebainika kuwa MSD imefanya ununuzi kwa zabuni nane huku upitiaji wa zabuni hiyo ukifanywa na mtu mmoja, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Zabuni zilizofikwa na hali hiyo ni za Sh milioni 134.4, dola 10,000 na Euro milioni 1.5.
Ulaji wa kutisha Bandari ya Dar es Salaam
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) iliingia mkataba na kampuni ya Singapore PTE Limited kwa ajili ya kuweka ‘Radio Data Terminals’ Februari 2010 wenye thamani ya dola 339,600. Punde tu baada ya TPA kupata radio hizo, mambo kadhaa yalianza kujitokeza.
Kwanza, menejimenti ikabaini kuwa ‘Radio Data Terminals’ hizo haziwezi kufanya kazi bila kile kinachoitwa kitaalamu kuwa ni ‘Access Points’ (virusha mawimbi). Hatua hiyo ikaifanya PTA iingie mkataba mwingine na Singapore PTE Limited Juni 21, 2010 kwa ajili ya kuweka virusha mawimbi 68 kwa gharama ya dola 399,000. Baada ya kununua vifaa hivyo, ikabainika tena kwamba haviwezi kufungwa juu minara ya iliyokuwapo. Kwa sababu hiyo, PTA ikaingia mkataba mwingine na CATS (T) Limited Septemba 17, 2010 kwa ajili ya kuweka minara mingine kwa gharama ya dola 133,000.
CAG anasema katika ukaguzi wake kwamba pamoja na kufanya yote hayo, bado ‘Radio Data Terminals’ hazikuweza kufanya kazi kama ilivyokusudiwa, kwa vile ilipaswa iunganishwe kwenye mkongo (fibre optic) kwa gharama ya dola 553,800 za Marekani. Kazi hiyo ikafanywa na EMEC.
Kwa kifupi, TPA ikajiingiza kwenye gharama za ziada za dola milioni 1.09 na bado kilichokusudiwa hakikuweza kupatikana kwa muda kutoka kwa mkandarasi aitwaye CATS. Hakuna gharama zozote ambazo TPA imeweza kuzidai kutokana na kucheleweshwa au kuingia gharama kubwa kiasi hicho. Hii inatiliwa shaka kuwa ndiyo ulaji wenyewe.
Sh milioni 100 zaliwa bila jengo la bosi TPA
TPA iliingia mkataba na kampuni ya AF MULT-CON LIMITED kujenga makazi ya Meneja wa Bandari Tanga kwa gharama ya Sh milioni 500. Utangazaji zabuni umebainika kuwa ulifuata taratibu zote. Hata hivyo, CAG amebaini kuwa kuna uzembe katika kufuatilia taratibu za mkataba wa zabuni. CAG mwenyewe alizuru eneo lililokusudiwa kujengwa jengo hilo, na hakushuhudia malighafi wala shughuli yoyote ya kuhalalisha malipo ya Sh milioni 100 ambazo tayari mzabuni alishalipwa.
Mkataba mwingine wa utata TPA
Wakati wa ukaguzi, CAG alibaini kuwa TPA iliingia mkataba na kampuni ya Chibeshi Construction kwa ajili ya kujenga uzio katika kitalu namba moja kwenye Bandari ya Mtwara. Mkataba huo ulikuwa na thamani ya Sh milioni 679.8. Ulitiwa saini Aprili 14, 2009 na ujenzi ulipaswa ukamilike kwa wiki 26 kutoka siku ya kutiwa saini mkataba.
Kabla ya mkandarasi kuanza ujenzi, TPA ikaamua kuvunja mkataba huo kwa maelezo kwamba hapakuwapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Uamuzi huo ukaifanya TPA iingie hasara ya Sh milioni 92.6 kama adhabu au faini. Ikamlipa mkandarasi. Fedha zikachukuliwa na mkandarasi bila kufanya kazi yoyote.
Mkataba mwingine wa utata waingiza hasara TPA
Katika ukaguzi, CAG amebaini kuwa PTA iliingia mkataba na kampuni ya WiA kwa ajili ya kuweka mawasiliano ya intaneti katika Makao Makuu ya TPA, na bandari nyingine zilizo chini ya Mamlaka hiyo. Mkataba huo ulikuwa wa miezi mitatu kuanzia Julai 2010. Hata hivyo, mradi huo haukukamilika baada ya muda uliopangwa kumalizika. TPA ikaamua kumwongeza mkandarasi muda hadi Februari 28, 2011 na mkandarasi bado alishindwa. TPA ilipaswa kumtoza mkandarasi kiasi cha dola 95,000 kwa kushindwa kutekeleza mkataba kwa muda, lakini haikufanya hivyo.
Hazina yalipa mamilioni ya mishahara hewa
Wakati wa ukaguzi, CAG amebaini kuwa Hazina imeendelea kutumia mamilioni ya shilingi kuwalipa wafanyakazi hewa katika taasisi mbalimbali. Katika ukaguzi huo, imebainika kuwa Chuo Kikuu cha Mkwawa (MUCE) kumekuwa na majina 42 ya watu wanaolipwa mishahara licha ya ukweli kwamba si watumishi wa chuo hicho. Imebainika kuwa kuanzia Oktoba 2009 hadi Juni, 2010 MUCE ilipokea Sh milioni 612 na kuwalipa watumishi hewa.
Katika Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Hazina imeendelea kuwalipa mishahara watu ambao si watumishi chuoni hapo. Baadhi ya waliostaafu na MNMA kupeleka majina yao Hazina, wanaendelea kulipwa. Hali hiyo imesababisha Sh milioni 134.74 zitumike kuwalipa watu ambao si watumishi katika chuo hicho. Fedha hizo hazikurejeshwa Hazina.
Katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, orodha ya majina kutoka Hazina inaonyesha kuwa hata wale ambao si watumishi tena wa chuo hicho, majina yao yapo kwenye orodha ya wanaostahili kulipwa mishahara. Kuanzi Oktoba 2010, Machi 2011, Mei 2011 na Juni 2011 Sh milioni 194.4 zimetumika kuwalipa watu ambao si watumishi katika chuo hicho.
Imebainika pia kwamba baadhi ya watumishi waliojiuzulu au kuacha kazi katika Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW), majina yao yameendelea kuwa kwenye orodha ya Hazina ya watumishi wanaopaswa kulipwa. Sh milioni 181 zilikuwa zimetumika kuwalipa hadi wakati ambao CAG alikuwa akiandaa ripoti hii.
Katika Chuo cha Elimu Dar es Salaam nako mambo ni kama hayo. Watu 56 ambao hawapo kwenye utumishi wameweza kulipwa Sh milioni 778.7 licha ya ukweli kwamba hawapo chuoni hapo. Hakuna rekodi inayoonyesha kuwa fedha hizo zilirejeshwa Hazina.
Fedha za Mifuko ya Jamii hatarini
Ukaguzi umebaini kuwa upo udhaifu mkubwa na hatari ya kupotea kwa mabilioni ya shilingi zilizowekezwa na Mifuko ya Jamii katika miradi mbalimbali nchini.
Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limetumia Sh bilioni 234.054 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma. Kati ya fedha hizo, ni Sh bilioni 35.218 pekee ambazo zilisainiwa katika ujenzi wakati wa awamu ya kwanza. Fedha zilizotolewa katika ujenzi wa awamu ya pili, hazikusainiwa. Majengo ya awamu ya kwanza yamekamilika, lakini Serikali haijaanza kurejesha fedha inazodaiwa na NSSF zenye riba ya Sh bilioni 14.157.
Wabunge waondolewe kwenye Bodi
Kwa mara nyingine, CAG amependekeza wabunge wasiwemo kwenye Bodi za Mashirika ya Umma na bodi nyingine. Anasema mapendekezo hayo yanatokana na ukweli kwamba kuwamo kwao kwenye bodi husababisha mgongano wa masilahi.
Anasema ni Tanzania pekee ambayo wabunge ni wajumbe katika bodi za mashirika ya aina hiyo. Utaratibu kama huo haupatikani mahali kwingineko duniani wala katika vyombo ambavyo Tanzania ni mwanachama.
Uteuzi wa wajumbe wa Bodi
CAG anatoa mapendekezo kwamba maofisa watendaji wakuu wa kampuni/mashirika ni vizuri wakateuliwa na Bodi za Wakurugenzi badala ya utaratibu wa sasa, ambako ni Rais anayewateua. Anapendekeza Rais aachiwe madaraka ya kuteua mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi.
Mapendekezo hayo, kwa mujibu wa CAG, yanalenga kuifanya Bodi ya Wakurugenzi iweze kuisimamia vema menejimenti na kuleta mabadiliko yanayotarajiwa.
Serikali ibane ununuzi mashangingi
CAG anapendekeza kuwa ili fedha nyingi zielekezwe kwenye maendeleo, Serikali haina budi kuweka utaratibu madhubuti wa kudhibiti matumizi hasa kwenye ununuzi wa magari ya kifahari, gharama za semina na kupunguza idadi ya wanaosafiri kwenye misafara ya viongozi ndani na nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment