.

.

.

.

Monday, April 01, 2013

VIJANA WA UPANGA NA BENDI ZA MIAKA YA THEMANINI



Upanga ni eneo muhimu sana katika historia ya muziki Tanzania. Hata katika miaka ya karibuni kulizuka kilichoitwa East Coast, muungano fulani wa wasanii wa Bongoflava toka maeneo ya Upanga, hii haikuwa mara ya kwanza kwa Upanga kuwa na wanamuziki waliotingisha mji. Enzi hizo za muziki wa soul, vijana wa Upanga walilipa eneo hili la mji jina la Soulville.Kwenye kona ya barabara ya Mindu na United Nations, nyumbani kwa familia ya Jengo, hapo ndipo palikuwa mahala pa mazoezi pa kundi lile la Groove Makers. Baadhi ya wanamuziki wa kundi hili walikuwa Mohamed Maharage, Joseph Jengo, Emmanuel Jengo, Herbert Lukindo, Willy Makame, na mpiga Drums ambae mpaka leo yupo katika anga za muziki Jeff. Kipindi hiki kilikuwa ni wakati wa muziki wa soul na kundi hili lilikuwa kundi la ubora wa juu wakati huo. Upanga ilikuwa na kundi jingine The Strokers, hili lilikuwa na awamu mbili, awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Donald Max, David Max, Harry Chopeta, Vincet Chopeta, Pino Makame na Ochiwa na Freddy Lukindo.

Awamu ya pili ya kundi hili lilkuwa na Sajula Lukindo,Onesmo Kibira,Innocent Galinoma,Ben Galinoma, Denis Pad,Francis Kasambala,Vicent na Harry Chopeta, Ally Mwarabu, Sabri Mmanga na wengineo. Barlocks ni Bendi nyingine 

iliyochipukia Upanga, jina la Barlocks lilitokana na kuweko kwa kundi laBarkeys ambalo leo linaitwa Tanzanites.Barlocks walikuwa wakitumia vyombo vya Barkeys kwani kwa wakati huo bendi hizi zilikuwa kama mkubwa na mdogo. Barlocks hiyo ya awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Jimmy Jumba,Pimbi Sokoine, huyu alipewa jina la utani Pimbi kutokana na kuwa mrefu sana, Said Mbonde kaka yake Amina Mbonde mwanamuziki mwingine muimbaji,Sajula Lukindo, Abraham. Kulikuweko na makundi mengine mengi hapo Upanga, kamaWhite HorseAquarius hapa walikuweko producer maarufu Hendrico Figueredo, Joe Ball,Joel De Souza, Mark De Souza,Roy Figueredo, Yustus Pereira,Mike De Souza. Baadhi ya wanamuziki wake walienda na kuungana na wengine Arusha na kuvuma sana na kundi la Crimson Rage, baadae wakarudi Dar na kujiita Strange. Baadhi ya kumbi walizokuwa wakipiga zilikuwa DI, Marine,Gymkhana,Maggot, St Joseph na kwenye shule mbalimbali. 

(Picha ya juu-Emmanuel 'Emmy' Jengo, Joseph 'Joe' Jengo, Herbert 'Herby' Lukindo. Kati-Jeff 'Funky' nyuma yake ni Willy Makame. Picha ya chini Willy Makame)



























Kwa Hisani ya Mzee Kitime

No comments:

Post a Comment