.

.

.

.

Friday, September 26, 2008

MTIKILA AJERUHIWA KICHWANI NA KUSHONWA NYUZI

HALI imezidi kuwa mbaya kwenye kampeni za uchaguzi wa mbunge na diwani wilayani Tarime, baada ya Mwenyekiti wa chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila kupigwa mawe na kujeruhiwa baada ya kudai kwenye mkutano wa hadhara kuwa Chadema ilimuua mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Chacha Wangwe.
Mashambulizi hayo yamekuja siku moja baada ya Kamanda wa Operesheni ya Jeshi la Polisi, Venance Tossi, kutangaza kuwa atatumia nguvu kudhibiti wafuasi wa vyama vya upinzani -Chadema na CUF- kwa madai kuwa wana vurugu, na pia ikiwa ni siku moja baada ya kiongozi wa Chadema kuuawa kwa risasi katika mapigao yanayodaiwa kuwa ya ukoo.
Mtikila, ambaye ni maarufu kwa kutoa tuhuma kali bila ya woga, aliwahi kutoa tuhuma hizo kwa Chadema mapema mwezi huu, akihusisha kifo cha mbunge wa jimbo la Tarime na mgongano wa kikabila ndani ya chama hicho na kumuhusisha mfanyabiashara mmoja maarufu.
Lakini jana, hakupewa nafasi ya kuendelea na tuhuma hizo kwa Chadema na badala yake wale waliokuwa akiwahutubia waliamua kumshambulia kwa mawe na kumjeruhi kiasi cha kushonwa nyuzi saba.
Mchungaji huyo wa makanisa ya ufufuo alikuwa ameanza kueleza kifo cha Wangwe ambaye alifariki kwenye ajali ya gari ndogo wakati akisafiri kutoka Dodoma kuelekea Dar es salaam kuhudhuria mazishi ya mfanyabiashara Bhoke Munamka.
Wakati akiendela kuwahutubia wananchi na kuituhumu Chadema kuwa ndio iliyomuua mbunge huyo wa zamani wa jimbo hilo, ghafla alipondwa na jiwe baada ya kuwa amegeukia upande wa kulia na hivyo kujeruhiwa
kichwani.
Shambulizi hilo lilisababisha mkutano huo wa hadhara kukatishwa wakati wasaidizi wake walipoanza harakati za kutafuta usafiri wa kumkimbizia hospitali ambako alitibiwa na kushonwa nyuzi saba.

No comments:

Post a Comment