MASHABIKI wa soka katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Morogoro, Dodoma na Arusha wamewasili jijini tayari kushuhudia mpambano wa mahasimu hao utakaopigwa Kesho kwenye Uwanja Mkuu jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.
Mmoja wa mashabiki hao, Mohamed Mpili, alisema kuwa amewasili jijini Dar es salaam akitokea Mtwara, lakini wakati anaondoka kulikuwa na mashabiki waliokodisha mabasi kwa ajili ya mchezo huo.
”Nimeacha watu wanajipanga kuja na mabasi mawili, Akida na Najmunisa...watu wamepania kwelikweli, kila mmoja ana itikadi yake sasa sijui wakati wa kurudi watarudi pamoja,” alisema shabiki huyo alipokutana na Msemaji Makao Makuu ya Yanga, Jangwani.
Jana Msemaji aliyekuwa katika kituo cha mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam, alishuhudia baadhi ya wasafiri waliokuwa wamevalia ’kimichezo’ wakiwasili katika mabasi mbalimbali na kuamini ni kati ya mashabiki hao wanakuja kwa mpambano huo.
Mashabiki zaidi ya 15 kutoka Tanga wakiongozwa na mwenyekiti wa matawi ya Simba, Tanga, Mbwana Msumari walitarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam jana mchana kwa basi la Raha Leo kwa ajili ya kuipa nguvu Simba kwa mchezo huo utakaofanyika kwenye Uwanja Mkuu wa Tanzania.
Mwenyekiti wa Tawi la Simba la Tanga lenye maskani yake barabara ya 16 Jijini hapa, Mbwana Msumari, alisema kabla ya kuanza safari: "Wanachama wa Simba Tawi la Tanga wameamua kutuma ujumbe wa wapenzi 15 nitakauongoza mimi, tumetumwa kwenda kushughulikia masuala ya kuhakikisha timu yetu inapata ushindi dhidi ya Yanga."
Mwenyekiti huyo alisema Tawi hilo limefikia maamuzi hayo kutokana na hali halisi ilivyochafuka katika klabu yao ya Simba na kwamba ikiwa wataendelea kuwaachia viongozi waliopo Dar es saalam kuna hatari ya kufungwa.
Pambano hilo ni la kwanza na aina yake kwenye Uwanja Mkuu wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment