
Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), limeanza kutekeleza masharti yaliyowekwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), ili kuhakikisha inajinasua na ndege zake zinarejea angani baada ya kuzuiwa kwa kushindwa kutimiza masharti ya usalama. Wakati ikikiri kuwa ndege zake zimepigwa marufuku kwa muda usiojulikana kuonekana angani, ATC imewaomba radhi wateja wake kwa kushindwa kutoa huduma kutokana na hatua hiyo ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga. Juzi, ilibainika kuwa ATC wamezuiliwa kurusha ndege zao kuanzia Jumatatu wiki hii kwa sababu wameshindwa kutimiza masharti ya kanuni za usalama wa ndege za TCAA ambayo ndiyo inasimamia usalama wa ndege kwa niaba ya serikali. Mkurugenzi Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa ATC, David Mattaka, jana alikiri katika mkutano na wanahabari ofisini kwake Dar es Salaam kuwa shirika hilo limezuiwa kurusha ndege zake baada ya kushindwa kutimiza masharti ya viwango vya usafiri wa anga vya TCAA, hivyo kusimamishwa kuanzia Jumatatu wiki hii. Alisema ukaguzi uliofanywa Desemba mwaka jana na Shirika la Kimataifa la Ukaguzi wa Usafiri wa Anga (IOSA), wakaguzi waligundua dosari 482 katika operesheni za ATC, ambazo zilitakiwa kurekebishwa. Aliyataja maeneo ya kasoro hizo ni kwenye muundo na menejimenti, ndege, usafirishaji, matengenezo, chumba cha marubani, usimamizi wa mizigo na operesheni za kiusalama. Alisema kutokana na hilo, waliajiri kampuni mbili za kimataifa, moja ya Afrika Kusini na nyingine, Air France, kuzifanyia kazi dosari hizo, na kwa sasa nyingi ya kasoro hizo zimerekebishwa na nyingine zinatarajiwa kukamilika katika wiki ya mwisho ya mwezi huu. Lakini alisema ukaguzi uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) kwa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania mwezi uliopita, ndio uliogundua dosari katika hati za kanuni za ATC, hivyo kutoa uamuzi wa kusimamishwa. “Novemba mwaka huu, ICAO ilikuja kufanya ukaguzi kwa TCAA jinsi inavyoendesha jukumu lake la kusimamia operesheni za ndege nchini. Katika ukaguzi huo waligundua kuwa hati za utaratibu zilizokuwapo TCCA hazikuwa zinaendana na taratibu za TCAA za mwaka 2006,” alisema Mattaka na kuongeza: “Hati hizo ndizo zile zilizokuwa zikiandaliwa kwa nia ya kuhakikisha zinaendana na kanuni mpya. Kwa hiyo, waligundua kuwa cheti cha usalama wa ndege kilichotolewa kwa ATCL na kilichokuwa kikitarajiwa kumalizika muda wake Desemba 15, 2008, kutokidhi haja ya kisheria. “Kwa hiyo, TCAA iliamua kukifuta cheti hicho hadi wakati ambao ATCL itakamilisha hati za utaratibu zitakazokidhi sheria ya TCAA.” Mattaka alisema tayari ATC imepeleka hati hizo kwa mamlaka hiyo juzi kwa sababu urekebishaji wa hati hizo ulikuwa umefikia hatua za mwisho, na wana imani watarejeshewa cheti chao katika siku chache zijazo. Alisema kwa mujibu wa TCAA, wanahitaji siku 10 za kazi kuweza kupitia hati hizo ili kuliwezesha shirika hilo la muda ambalo kwa miaka ya karibuni limekuwa katika wakati mgumu, kurusha tena ndege zake. “Napenda kusisitiza kwamba suala hilo halina uhusiano na usalama wa abiria, hakukuwa na athari kwa abiria. Niwatake radhi abiria wetu waliokuwa tayari kusafiri na ndege zetu na wale ambao waliotarajia kusafiri,” alisema. Akizungumzia hasara, Mkurugenzi Mkuu huyo wa ATC alisema kubwa ni usumbufu kwa wateja waliokuwa watumie ndege zao, ingawa kwa wiki wamekuwa wakiingiza mapato ya Sh milioni 300. Alisema kwa wateja waliokuwa wasafiri hivi karibuni, wamewarejeshea fedha zao, huku akionyesha shukrani kwa serikali hasa kwa Rais Jakaya Kikwete, kwa jinsi anavyopigania kuhakikisha shirika hilo linaondokana na matatizo iliyonayo. “Kwa kweli serikali inatusaidia sana na kutuunga mkono na hasa Rais Kikwete amekuwa mstari wa mbele. Najua ipo mipango ya ama kutusaidia kwa kutupa fedha ingawa hili ni gumu kwa sababu vipaumbele ni vingi, lakini pia liko la kutafuta mwekezaji. Serikali inayaangalia hayo yote,” alisema Mattaka. Alipoulizwa kama anao uwezo wa kuliokoa shirika hilo na endapo hafikirii kuwa limemshinda na ajiuzulu, Mattaka alijibu, “Meneja yeyote mzuri, anaweza kuendesha biashara yoyote.” Alisema kuendesha shirika la ndege ni kazi ngumu kwa sababu ya gharama na akatoa mfano kuwa kati ya Juni hadi Agosti, ndege zake, Air Bus ilikuwa inatumia Sh milioni tisa kwa safari ya Dar-Mwanza-Dar, huku safari hiyo kwa Boeing ikigharimu Sh milioni 10 na kwa Dash 8, ikitumia Sh milioni tatu. ATC ni shirika pekee la ndege la umma, na hadi Mei mwaka huu, lilikuwa na ndege sita, tatu zikiwa ni mali yake yenyewe na nyingine za kukodi. Hivi karibuni, Kamati ya Kudumu ya Miundombinu ya Bunge ilieleza kwamba kulikuwa na mpango wa shirika hilo kuingia ubia na shirika moja la ndege la China.
No comments:
Post a Comment