MBUNGE wa jimbo la Kyela (CCM), Dr. Harrison Mwakyembe amenusurika kufa baada ya gari yake aliyokuwa akisafiria kupata ajali mbaya.
Ajali hiyo ilitokea jana, majira ya saa 1.10 asubuhi katika eneo la mteremko mkali wa Ihemi, karibu na kijiji cha Tanangozi, wilayani Iringa, Mkoani Iringa.
Shangingi la Mbunge huyo aina ya Toyota Landcruiser, lenye namba za usajili T362ACH, lililokuwa likiendeshwa na Joseph Msuya (30), liliacha njia umbali wa mita sitini kutoka barabarani kabla ya kugonga mti na kuug’oa kisha kupinduka.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Advocate Nyombi, gari hilo lilipata ajali hiyo baada kukanyaga shimo na tairi la upande wa kulia kuchomoka ndipo dereva alipopoteza mwelekeo na gari kwenda nje ya barabara upande wa kushoto na hatimaye kugonga mti na kupinduka.
"Taarifa za awali zinaonesha kuwa ajali hiyo ilitokea wakati dereva wa Mbunge huyo akilipita lori kabla ya kukanyaga shimo hilo," alisema.
Kamanda Nyombi alisema Dk Mwakyembe aliokolewa na wasamaria wema pamoja na askari wa usalama barabarani wawili waliokuwa kwenye basi dogo lililokuwa linakwenda Njombe na kukimbizwa katika hospitali hiyo.
Mbunge huyo amelazwa wodi namba tano ya Grade one ya Hospitali ya Mkoa wa Iringa na hali yake inaendelea vema. Mwandishi huyu alipofika hospitali ya Mkoa wa Iringa, alishuhudia maafisa wengi wa usalama wa Taifa pamoja na maafisa wengine wa serikali wakiwa nje ya wadi 1B alimokuwa amelazwa.
Hata hivyo, waandishi na watu wengine walikuwa hawaruhusiwi kabisa kuingia ndani ya chumba alichokuwa amelazwa isipokuwa madaktari na wauguzi.
Hali iliendelea kuwa tete huku taarifa zikivuma kuwa Dr.Mwakyembe amepoteza maisha hususani baada ya mtumishi wa Mungu na Mkurugenzi wa shule za Kimataifa za Star za Iringa, Jesca Msambatavangu kuruhusiwa kuingia kumwombea Mbunge huyo.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Mkoa wa Iringa, Dr.Oscar Gabone, aliwaambia waandishi wa habari baadaye kuwa hali ya Mbunge huyo haikuwa mbaya kama taarifa zilizokuwa zinaenezwa. "Uchunguzi wa awali unaoenesha ameumia taya la kulia, hata hivyo halijavunjika na muda wowote kuanzia sasa anaweza kupelekwa katika hospitali kubwa za jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi," alisema.
Alipoulizwa kwa nini waandishi hawaruhusiwi kumwona alisema kuwa wangeruhusiwa baadaye kwa maelezo kuwa kwa muda huo alikuwa anapumzika.
Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa alisema Dk Mwakyembe aliondoka juzi jioni majira ya saa mbili usiku jimboni kwake Kyela na alilala Makambako wilayani Njombe mkoani Iringa na kwamba jana alfajiri aliendelea na safari yake ya jijini Dar es Salaam kabla hajapata ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment