MBUNGE wa Kyela (CCM), Dk Harrison Mwakyembe ameitupia kombora CCM kwamba, baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hicho, wameamua kumhujumu kwa kupeleka fedha za rushwa katika jimbo lake ili kumng'oa.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumapili, Mwakyembe alisema viongozi hao wamekuwa wakishirikiana na jopo la mafisadi kusambaza fedha hizo kwa wananchi wa Kyela.
Alisema hivi karibuni wabaya wake hao waliingiza mamilioni ya fedha katika jimbo hilo, zilizopelekwa na kiongozi Mwandamizi wa CCM Mkoa wa Mbeya, lakini alipewa taarifa na kuwataka wazee wazipokee na kuzitumia kwa vile ni fedha zao zilizoibwa na mafisadi.
"Mimi nimewashauri wananchi wazipokee fedha hizo na wazitumie kwa sababu ni mali yao iliyoporwa na mafisadi," alisema.
Mwakyembe alisema anashangaa kuona kwamba rushwa inayopelekwa katika jimbo lake na kusambazwa na mafisadi inajulikana na viongozi wa serikali na CCM, lakini hakuna hatua yoyote ambayo imechukuliwa mpaka sasa.
"Serikali ina vyombo vya dola inaweza kuchunguza, lakini mpaka sasa hakuna hatua zilizochukuliwa kwa wahusika," alisema.
Alisema njama za watu hao zinafanywa zikiwashirikisha pia baadhi ya viongozi wa serikali waziwazi bila ya kificho, hali ambayo inamfanya aamini kuwa wabaya wake wana baraka na wanayoyafanya.
No comments:
Post a Comment