.

.

.

.

Monday, October 24, 2011

ALBINO AFANYIWA UNYAMA NA KUPOTEZA MKONO

MLEMAVU wa ngozi aliyekatwa mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana, Kulwa Lusana (16), amesimulia alivyojikuta akiwafukuza wavamizi hao, huku akilia na kuwaomba wamrudishie mkono wake.

Kulwa ametoa maelezo hyao Polisi jana na kuongeza kuwa juhudi hizo za kudai kurudishiwa mkono wake, hazikuzaa matunda, kwani wakataji hao walizidi kutokomea gizani na kumuacha akitapatapa.

Baada ya kupoteza matumaini ya kuupata mkono wake, Kulwa alisimulia kwamba akiwa anagugumia kwa maumivu makali, alikimbilia kwenye nyumba ya baba yake ambapo aligongana naye mlangoni na wote kuanguka chini.

Mlemavu huo alifanyiwa unyama huo juzi saa 7 usiku katika Kijiji cha Mbizi, Kata ya Segese wilayani Kahama katika Mkoa wa Shinyanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani alisema watuhumiwa hao walivunja mlango na kuingia ndani kwa albino huyo na kuanza kumshambulia na kumjeruhi sikio na baadaye wakakata mkono wake wa kulia na kuondoka nao.

Kwa mujibu wa Kamanda Athumani, albino huyo alipiga kelele ya kuomba msaada kwa baba yake, Lusana Nkola ambaye hata hivyo wakati akitoka katika harakati za kumuokoa mtoto wake huyo, alipigwa jiwe kichwani akaanguka chini.

Alisema baada ya kufanyiwa unyama huo, watu hao waliufunga mkono huo kwenye mfuko na kuanza kukimbia nao na kutokomea pasipo julikana na kumuacha albino huyo akigugumia kwa maumivu makali.

Kutokana na tukio hilo, Polisi inamshikilia Petro Nkola mkazi wa kijiji cha Mtukula Runzewe wilayani Bukombe ambaye ni baba mdogo wa mlemavu wa ngozi, Kulwa Lusana (16).

Hata hivyo, Kamanda Athumani hakutaka kueleza kwa undani sababu za kumshikilia baba huyo zaidi ya kufafanua kuwa ni kwa mahojiano zaidi na uwezekano wa kuwapata watuhumiwa wengine waliotoroka na mkono wa mlemavu huyo.

Kulwa kwa sasa yupo katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama akiuguza jeraha lake na hali yake inaendelea vizuri.

Kamanda Athumani aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa watu wote watakaowadhani kuwa ni washiriki wa tukio hilo la kinyama alilofanyiwa mtoto huyo.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku chache tu baada ya mlemavu mwingine wa ngozi, Adam Robert (14) kujeruhiwa kwa kukatwa na sime mkono wa kushoto na kunyofolewa vidole vya mkono wa kulia huko katika Kijiji cha Nyaruguguna wilayani Geita, mkoani Mwanza.

Katika tukio hilo la Geita, baba mzazi na mama wa kambo wa mtoto huyo, wanashikiliwa kwa tuhuma hizo

No comments:

Post a Comment