.

.

.

.

Monday, April 23, 2012

AKAMATWA NA MIHADARATI YA SHS. MIL.540

JESHI la Polisi Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya kimemkamata raia wa Ghana 
akiwa na kilo 12 za dawa ya heroin zenye thamani ya Sh milioni 540. 

Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACP), Godfrey Nzowa alisema ofisini kwake Dar es Salaam jana kwamba dawa hizo zimekamatwa kwenye sanduku la Kwaku Safo (41) saa 10 alfajiri akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA). 

Kamanda Nzowa alisema Safo aliyekuwa na hati ya kusafiria namba H 2289855 iliyotolewa Oktoba 3, 2008, alikutwa na kilo hizo za dawa za kulevya alizozificha ndani ya masanduku
mawili ya nguo akiwa tayari kusafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya iliyokuwa inaondoka saa 11:10 asubuhi. 

Safo aliingia nchini kama mtalii Aprili 18, mwaka huu na kufikia katika Hoteli ya Lorrate iliyopo Buguruni katika Manispaa ya Ilala. 

“Siku ya kuondoka tulipewa taarifa na wasamaria wema na kuanza kufuatilia nyendo zake mpaka tulipomkamata uwanja wa ndege, ambapo Polisi kwa kushirikiana na watumishi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege walifanikisha kumkamata,” alisema Nzowa. 

Alisema Safo atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika ili sheria ichukue mkondo wake. 

Hivi karibuni, Polisi iliwakamata raia wa Nigeria na Guinea Bissau wakiwa na kilo tatu za dawa za kulevya aina ya kokeini zenye thamani ya Sh milioni 128.5 wakiwa tayari kusafiri kwenda Bamako nchini Mali. 

Watu hao ni Mnigeria Joseph Chukwuemeka (47) aliyekuwa amemeza pipi 83 na Alberto Mendes (49) raia wa Guinea Bissau aliyekuwa amemeza pipi 85. 

Akizungumzia tathmini ya uingizwaji na upitishwaji wa dawa za kulenya katika mipaka ya Tanzania, Nzowa alisema tatizo hilo limepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na polisi kudhibiti mianya ya uingizaji na upitishaji.

No comments:

Post a Comment