.

.

.

.

Sunday, June 10, 2012

BOB NYANGA MAKANI AFARIKI DUNIA


MWASISI wa Chadema na Mwanasheria mkongwe nchini Bob Nyanga Makani, amefariki dunia usiku katika hospitali ya Aga khan, jijini Dar es Salaam.


Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, Makani alizidiwa ghafla saa 3: 00 usiku wa kuamkia leo na kukimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan ambako alifariki dunia saa 4.15 usiku.

“Amekuwa anaumwa muda mrefu, mara kadhaa akipelekwa hospitali na baada ya muda anaruhusiwa, lakini hii ya sasa alikua nyumbani akazidiwa ghafla wakampeleka hospitali na ilipofika saa 4.15 wakasema amefariki,” alisema Zitto.

Zitto alisema kuwa, suala la wapi utakapozikwa Makani ambaye ni Katibu Mkuu wa Kwanza na Mwenyekiti wa pili wa Chadema, litajulikana baada ya kujadiliana na familia ya marehemu.

“Suala la wapi atazikwa kama ni Shinyanga ama Dar es Salaam, litajulikana baada ya kuzungumza na familia yake, kwa sasa tunashughulika kwanza na kuhifadhi mwili wa mzee wetu,” alisema Zitto.
Zitto alisema msiba wa utakuwa nyumbani kwa marehemu eneo la Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

Kwa siku za hizi karibuni afya yake imekuwa ikizorota na kumfanya kuripotiwa kuanguka mara kwa mara alipokuwa akifanya shughuli zake.

Januari 17 mwaka huu katika msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema Regia Mtema, Makani alianguka muda mfupi baada ya kuuaga mwili wa marehemu.

 Baada ya tukio hilo, alibebwa na kupelekwa pembeni ambako alipepewa kwa takriban dakika tano kisha kurejea katika hali yake ya kawaida na kurudi kwenye kiti chake

Alikuwa Katibu Makuu wa kwanza wa Chadema kati ya mwaka 1993 hadi 1998, alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho kuanzia mwaka 1998 hadi 2004 na amegombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kwa mara tatu kati ya mwaka 1995 na 2000 na mwaka 2005.

Kazi ambazo amewahi kuzifanya serikalini; alikuwa naibu mwanasheria mkuu wa serikali, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 1966 na elimu yake ana shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu Cha Makarere nchini Uganda.
 


Mwananchi

No comments:

Post a Comment