.

.

.

.

Wednesday, September 05, 2012

BI KIDUDE APATA NAFUU

Na Mahmoud Zubeiry


HALI ya afya ya msanii mkongwe nchini, Fatuma Binti Baraka, maarufu kama Bi Kidude inaendelea vizuri katika hospitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam alipolazwa na wakati wowote kuanzia kesho anaweza kuruhusiwa kurudi nyumbani, ila familia imemstaafisha rasmi sanaa.
BIN ZUBEIRY alifika katika wadi namba 202 hospitali ya Hindu Mandal, jioni hii kumjulia hali Bi Kidude, mwimbaji maarufu na mkongwe haswa wa muziki wa Taarabu duniani na ‘alhamdulillah’, Bi Mkubwa anaendelea vizuri.
Watu wanapishana kuingia na kutoka kumsalimia Bi Kidude, wengine wakitoka nje ya nchi, baadhi mashabiki wake na baadhi ndugu na jamaa.
Lakini jambo moja tu Bi Kidude analaani vikali ni taarifa za kuzushiwa kufariki dunia mwishoni mwa wiki. “Watu wamenizushia kufa Zubeiry, na wewe hukuja kuniona, ulifikiri nimekufa? Mi mzima, si unaniona, cheki,”alisema Bi Kidude na kuuvuta mkono wa BIN ZUBEIRY kwa nguvu akiuminya ‘kibaunsa’ kuonyesha nguvu za misuli yake, kwamba yeye yuko mzima.
Bi Kidude alikuwa mcheshi wakati anazungumza na watu mbalimbali waliomtembelea hospitali na alimuambia BIN ZUBEIRY kwamba anasumbuliwa na maradhi ya sukari, ambayo ni maradhi yake kwa muda mrefu, ila yalimzidia kwa kukiuka taratibu za vyakula.
“Kweli nilikuwa naumwa, ngozi yote ilivuka hii, nilikonda sana, ila sasa Alhamdulillah mi mzima, mi mzima, naweza kuondoka,”alisema.
Mwonekano wa Bi Kidude ni mtu mwenye afya njema japokuwa amelala kitandani wadi namba 202, Hindu Mandal na sasa anainuka kwenda mwenyewe msalani.
Amezuiwa kuvuta sigara tangu alazwe hospitalini hapo na inaonekana kwa hamu ya sigara anaomba aondoke hata sasa hivi. Amewekewa waangalizi wawili, wa kike na wa kiume, wote wakiwa ni wanafamilia.
Hidaya Abdi Omar, mkwe wa Kidude ambaye ni mmoja wa waangalizi wake hospitalini hapo amesema kesho Bi Mkubwa huyo atafanyiwa vipimo ambayo kama vitakuwa namna ambavyo madaktari wa hospitali hiyo wanataka, ataruhusiwa.
Hidaya ni mke wa mtoto wa mdogo wake wa kiume Bi Kidude, aitwaye, Abdallah Baraka ambaye hivi sasa ni marehemu. “Bi Kidude hakubahatika kuzaa, lakini ndugu zake wamezaa, mimi ni mke wa mtoto wa kaka yake Bi Kidude, na kwa sasa ndiye naishi na huyu bibie kulingana utu uzima na hali yake pia,”anasema Hidaya.
Hidaya anasema msimamo wa familia umekwishapita kwamba Bi Mkubwa huyo sasa hataruhusiwa kufanya kazi yoyote ya sanaa, atakuwa wa kupumzika tu acheze na wajukuu.
“Hatapanda tena jukwaani popote, sasa basi tena, akae tu apumzike, familia imekwishaamua,”alisema. Familia hiyo hiyo imeamua Bi Kidude asipigwe picha yoyote akiwa wadini. 
Ndugu zake wote watatu ambao ni wadogo zake Bi Kidude wamekwishafariki dunia na kwa sasa Bi Kidude anakula matunda ya watoto wa ndugu zake hao, ambao kwa sasa ndio wanamlea.
Hakuna promota yeyote wa tamasha au kiongozi wa serikali, au chombo chochote cha sanaa aliyekwenda kumjulia hali Bi Kidude wadini, zaidi baadhi ya wasanii wanapiga simu tu na kwa hilo wala Bi Mkubwa huyo hajali, watu wanaokwenda kumuona na kumfariji kwake wanatosha.
Bi Kidude alianza kusumbuliwa na maradhi mwezi uliopita, lakini baadaye akapata ahueni na kufanya mahojiano hadi na vyombo vya habari, lakini ghafla mambo yakabadilika tena na amerudi hospitali, ila kwa sasa unaposoma habari hii yuko vizuri Hindu Mandal.
Bi Kidude ni gwiji wa muziki katika Bara la Afrika, katika fani ya muziki wa mwambao ambao hujulikana kwa jina la Taarabu. Muziki huu ambao ni mchanganyiko wa muziki toka nchi za Kiarabu na vionjo vya muziki wa Kiafrika umekita sana katika mwambao wa Afrika Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.
Fatuma binti Baraka au Bi Kidude, alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar katika familia ya watoto saba (7). Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara wa nazi, zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar. 
Bi Kidude anasema hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ana hakika ni kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya. 
Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 90.
Bi Kidude anasema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka 10 na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo Sitti Binti Saad. Anasema wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa wako karibu basi yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani kwa Bi Sitti, wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje, kule ndani Bi Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye huku nje alikuwa akimsikiliza kwa makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa akiimba. Aliendelea hivyo hadi akawa mahiri sana katika uimbaji.
Alipokuwa na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930, huko aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake uimbaji.
Bi Kidude hategemei kazi moja tu ya kuimba, kwani pia ni mfanyabiashara ya 'wanja' na 'hina' ambavyo anavitengeneza yeye mwenyewe, pia ni mtaalamu wa matibabu kwa dawa za mitishamba na zaidi ya hayo ni mwalimu mzuri sana wa 'Unyago' na ameanzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote hakuna aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.
Watu wanasema 'Utu uzima dawa' Bi Kidude ana upeo mkubwa sana wa akili kwani pamoja na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na tamaduni za kiarabu ambapo mwanamke anatakiwa wakati wote akiwa hadharani ajifunike, Bi Kidude aliliona hili katika upeo mwingine kwamba ni sheria tu ya kitamaduni toka Uarabuni, hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake, na sasa hivi anavaa kama Mtanzania na si kama Mwarabu. Lakini hakubakia hapo alivunja na miiko mingine zaidi ya kutokunywa na kuvuta, kwani Bi Kidude anakunywa pombe na kuvuta sigara jambo ambalo si kawaida kwa wanawake Zanzibar.
Bi Kidude amekwisha tembelea nchi nyingi sana ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.
Amekwisha pata tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 tuzo ni ya maisha. Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX ilienda kwake.
Nyimbo alizowahi kuimba ni pamoja na Muhogo wa jang'ombe, na anaimba kwa Kiswahili na Kiarabu. Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Quraan.



CHANZO CHA HABARI: BIN ZUBEIRY

No comments:

Post a Comment