.

.

.

.

Friday, April 25, 2014

RAIS JK AWAKA MOTO

Rais Jakaya Kikwete ameagiza kuimarishwa kwa udhibiti katika viwanja vya Ndege vya Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (Kia), kutumiwa kupitisha dawa za kulevya kwenda nje na kuingia nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la tatu la abiria JNIA, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema hajaridhishwa na kasi ya udhibiti wa dawa za kulevya katika viwanja hivyo.
Alisema inashangaza dawa za kulevya zinapita katika viwanja hivyo na watendaji wote wapo na zinakwenda kukamatiwa Afrika Kusini.
“Sijaridhishwa, unasikia kila siku mtu amekamatwa Afrika Kusini na dawa za kulevya, sijui mwanamuziki gani, siridhishwi hata kidogo,” alisema.
Rais Kikwete alimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Mhandisi Suleiman Suleiman kuhakikisha mianya hiyo inazibwa vinginevyo ataanza kumwadabisha yeye kisha wengine watafuata... “Nitaanza na wewe mkurugenzi na mwenyekiti wako wa bodi. Mtu anakuja hapa, sijui mwanamuziki gani, mara yoo...yoo... kwa kuwa mnamfahamu anapita, hatuwezi kuwa namna hiyo.”
Aliagiza apewe orodha ya majina ya maofisa wanaodhaniwa kujishughulisha na biashara hiyo naye atawaondoa kwa kuwa sheria inamruhusu... “Rais hashtakiwi, nitawaondoa, nipeni majina kwa kuwa kinachotokea hivi sasa kinaonyesha wote tunafanya biashara ya dawa za kulevya, wengine inatuumiza sana tunaonekana wote ndicho tunachofanya.”
Alibainisha kuwa haingii akilini kusikia kuna kitu kinakwamisha udhibiti wa dawa hizo katika viwanja hivyo ikiwamo Sheria ya Ununuzi wa Umma... “Miaka miwili hiyo sheria gani kwa kitu cha Sh2.5 milioni... je, ingekuwa Sh600 milioni si ndiyo kungegeuzwa gulio?” alihoji.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alifafanua baadaye kuwa Rais alikuwa anazungumzia kuchelewa kufungwa kwa mfumo wa kubaini dawa za kulevya uwanjani hapo, kutokana na mchakato mrefu wa sheria hiyo.
Jengo la abiria
Rais Kikwete alisema atahakikisha Hazina inatoa fedha zinazotakiwa kuharakisha ujenzi wa jengo hilo la abiria ambalo litakuwa na maegesho ya ndege 18 kwa wakati mmoja, litakalohudumia abiria milioni sita kwa mwaka badala ya milioni 2.5 wa sasa.
Mradi huo ambao unatekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya Kimataifa ya BAM ya Uholanzi, utagharimu Sh518 bilioni na Serikali iliahidi kutoa asilimia 50 ya fedha hizo sawa na Sh89 bilioni huku kiasi kingine kikitolewa na Serikali ya Uholanzi.
Hata hivyo, hadi sasa fedha hizo hazijatolewa jambo ambalo liliwahi kulalamikiwa na Mkurugenzi wa TAA kwamba linakwamisha ujenzi huo.

No comments:

Post a Comment