RAIS mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa amevijia juu vyombo vya habari nchini kwa kile alichodai vimekuwa vikimnukuu vibaya na kupotosha ukweli wa mambo. Bw. Mkapa alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki,katika sherehe za Jubilee ya kutimiza miaka 100 ya Usista ya Kanisa la Mtakatifu Benedict lililopo Ndanda, wilayani Masasi. Katika sherehe hizo Bw.Mkapa ambaye alikuwa mgeni rasmi, alitumia fursa hiyo kukanusha habari zilizochapishwa na kutangazwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni kuwa ameamua kuachana na siasa na kwamba sasa anajihusisha zaidi na masuala ya dini. Alisema kuwa hana nia ya kujihusisha na masuala ya dini zaidi kama kuwa kiongozi wa kanisa na kwamba yeye ni muumini sawa na waumini wengine, hivyo hakuna tofauti kati ya awali na anavyojihusisha sasa na masuala hayo nakusisitiza kwamba vyombo vya habari vilimnukuu vibaya. "Nilikuwa Chato, mkoani Kagera, baada ya hapo nilipitia Mwanza…niliporudi nyumbani mwanangu akaniuliza baba siku hizi unataka kuwa kiongozi wa kidini?...Nikamuuliza kulikoni? ...akanijibu magazeti yameandika hivyo," alisema Bw.Mkapa. "Kweli siku ya Pili nikakuta katuni kwenye gazeti ikiwa imebeba vitabu na Biblia…sasa nataka kuwahakikishia kuwa sitaki uaskofu wala siuhitaji…mimi ni mcha Mungu wa kawaida kama nilivyokuwa awali” alisisitiza Bw.Mkapa
No comments:
Post a Comment