MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah amekoleza moto wa mjadala wa Bunge kuhusu utendaji wa taasisi yake baada ya kujitokeza hadharani na kueleza kuwa hana mpango wa kujiuzulu.
Na kama haitoshi, Dk Hoseah amesema wabunge hawamtaki, wapige kura za kutokuwa na imani naye, ikiwa ni siku mbili kabla ya Bunge kujadili taarifa ya serikali ya utekelezaji wa maazimio ya chombo hicho kesho, kama alivyoahidi Spika Samuel Sitta.
Katika maazimio hayo kuhusu kashfa ya utoaji umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond Development LLC, Dk Hoseah anatakiwa kuwajibishwa na mamlaka ya juu kutokana na taasisi yake kushindwa kubaini rushwa katika utoaji wa zabuni hiyo.
Hoseah, aliyeitisha mkutano na waandishi wa habari ambao kila mmoja alipewa kipeperushi kinachotoa ufafanuzi wa athari za malipo yasiyostahili kwa watumishi wa umma na adhabu zake, alionekana ni mwenye jazba, msimamo na kujiamini, licha ya joto la uchunguzi huo na shinikizo la wabunge kutaka awajibishwe, kuwa juu.
Akijibu swali kwamba kwanini asijiuzulu ili kuonyesha uadilifu baada ya maafisa wenzake waandamizi wa serikali waliotajwa katika Richmond kung'oka, Dk Hoseah alianza kuhoji: "Kwanini unataka nijiuzulu.
"Sasa nakwambia, sina mpango wa kujiuzulu siwezi kujitia kamba eti ili nionekane mzalendo bila kosa, kwanini unataka nijiuzulu au unataka kuchukua nafasi yangu?"
Hadi sasa, serikali haijaeleza kama imeshawashughulikia maofisa waandamizi waliotakiwa kuwajibishwa na mamlaka za juu, lakini katika kipindi cha miezi michache iliyopita, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Johnson Mwanyika na Arthur Mwakapugi, aliyekuwa katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini walistaafu kwa mujibu wa sheria.
Kauli ya Dk Hoseah inakuja wakati Takukuru ikishutumiwa kuwa inaendesha uchunguzi kuhusu malipo ya posho mbili dhidi ya wabunge kwa lengo la kuwashughulikia wale ambao wamekuwa mstari wa mbele kutaka serikali imwajibishe kutokana na uhusika wake kwenye kashfa ya Richmond.
Kashfa hiyo ya Richmond tayari inaonekana kusababisha msuguano mkubwa kati ya Bunge na Serikali, kiasi cha kusababisha watendaji wakuu wa taasisi hizo kutofautiana misimamo.
Huku kukiwa na ongezeko la kilio cha kutaka awajibishwe, Dk Hoseah alisema: "Nihukumiwe kwa haki si kwa hisia. Kosa langu nini katika Richmond, taarifa ya pili ya azimio namba 20 la Kamati ya Nishati na Madini bungeni iko wazi... lakini nasema uchunguzi dhidi ya wabunge utaendelea na naomba watoe ushirikiano; waiache Takukuru ifanye kazi zake; waonyeshe uongozi wa mfano na uadilifu kama ambavyo wamekuwa wakipambana na ufisadi."
Kumbukumbu za Bunge (Hansard), kuhusu Taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini ya Agosti mosi, kujibu taarifa ya serikali iliyotolewa Julai 25, inasema: "Mheshimiwa Spika, Azimio Na. 20, Serikali iendeshe uchunguzi maalum ili kubaini ukweli kama taarifa rasmi ya Takukuru iliyotoa matokeo ya uchunguzi kuhusu mchakato wa Richmond ilikataliwa na kuharibiwa na kutolewa nyingine.
"Na kama jalada halisi linalohusu kampuni ya Richmond lililokuwa BRELA liliharibiwa na kuwekwa jingine kwa lengo la kuficha ukweli. Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa Serikali: Kamati ya Vyombo vya Dola imekamilisha uchunguzi wake kuhusiana na suala hili.
"Na imebainika kuwa, si kweli kuwa taarifa rasmi ya Takukuru iliyotoa matokea ya uchunguzi kuhusu mchakato wa suala la Richmond ilikataliwa na kuharibiwa na kutolewa nyingine kwa lengo la kuficha ukweli.
"Vile vile, taarifa ya kamati ya vyombo vya dola inaonyesha baada ya upelelezi na uchunguzi wa kina kufanyika wameridhika kuwa jalada halisi la Richmond lililokuwa BRELA halikuharibiwa na wala hakukuwa na jalada lingine lililowekwa kuficha ukweli wa jambo hili."
"...Maoni ya Kamati; Kamati inaridhika na taarifa hiyo."
Hoseah akitumia azimio hilo, alisema alibahatika kusoma kwa makini taarifa zote za kamati kuanzia ya kwanza na hiyo ya pili na kuhoji : "Sasa nijiuzulu kwa kosa lipi, watu mnihukumu kwa haki, au unataka kuchukua nafasi yangu (alimuuliza mwandishi wa gazeti hili)?"
Alisema kwa kipindi chote atakachokuwepo katika uongozi, atasisimamia sheria na hakuna aliye juu ya sheria na kuongeza: "Watu waache danganya toto, hakuna kisasi ni usimamizi na utekelezaji wa sheria tu."
Dk Hoseah alifafanua kwamba, tayari suala hilo la kuwajibishwa liko mamlaka ya juu (rais), hivyo ni vema wakasubiri maamuzi na kusisitiza kwamba, "uchunguzi huo utaendelea kwa hiyo waheshimiwa wabunge, wazee wangu toeni ushirikiano ili suala hili lisije kutufikisha pabaya, nchi hii ni ya amani".
Mkuu huyo alitumia mkutano huo kufafanua pia kwamba, uchunguzi huo haukumlenga mtu yeyote ambaye ni mjumbe wa kamati iliyochunguza kashfa ya Richmond, akisema: "Kwanini, mbona Mheshimiwa Zitto (Kabwe) tumemhoji, yeye alikuwa kamati ya Richmond?"
Hoseah alisema ombi la kufanywa uchunguzi huo ni la Bunge lenyewe kupitia barua ya Februari 26, 2008, ambayo ilimtaja yeye kwa jina ikimtaka afanye uchunguzi huo na kuhoji: "Kwa hiyo Bunge lenyewe linaweza kuandika barua kutaka kuwalenga watu fulani?"
Spika Sitta alishaeleza kuwa hafahamu lolote kuhusu uchunguzi huo na kuitaka serikali isitishe zoezi hilo, huku Waziri Mkuu Mizengo Pinda akieleza kuwa suala hilo linatokana na maagizo ya ofisi ya rais.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba kinachofanyika ni uchunguzi na haimaanishi wabunge wamethibitika kula posho mara mbili na kuongeza: "Sasa si ndiyo vizuri,... kwanza tunawapa haki nao kuwasikiliza, maana inawezekana mwisho wa siku ikibainika ni taarifa feki."
Kuhusu malalamiko ya wabunge kudhalilishwa na kuhojiwa na vijana wadogo wa taasisi hiyo, alipinga akisema si kweli na kuongeza: "Afisa ambaye anasimamia jambo hili ni mchunguzi mkuu ambaye amekuwa katika fani hii tangu mwaka 1973... kwa umri alionao hadi sasa anatarajia kustaafu mwakani."
Hata hivyo, awali akijibu maswali mengine, kama tatizo ni baadhi ya wabunge hawataki kuona sura yake (Hoseah) basi ni vema wakapiga kura ya kutokuwa na imani naye.
"Kama ulivyosema tatizo ni Hoseah hawajadili Takukuru, basi kama hawataki kuona sura yangu wapige kura ya kutokuwa na imani na mimi," alisisitiza.
No comments:
Post a Comment