.

.

.

.

Thursday, November 13, 2008

KUIUMBUA KAGODA NI SAWA NA KUIUMBUA NCHI !!!!

WAKATI watuhumiwa 20 wakiwa, hadi juzi, wamekwisha kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT), ushahidi mpya umeibuliwa unaoonyesha kwamba kampuni ya Kagoda Agricultural Limited, ambayo wahusika wake bado hawajashitakiwa, ilikuwa ya kwanza kuchota mapesa hayo zaidi ya miaka minane iliyopita. Uchunguzi wa muda mrefu wa Raia Mwema umethibitisha kuwapo kwa uhusiano mkubwa kati ya kampuni ya Afritainer (T) Limited na kampuni ya Kagoda Agricultural Limited ambayo hadi sasa wahusika wake na mahali ilipo ni kitendawili. Kampuni ya Afritainer ilifanikiwa kuchota zaidi ya Shilingi bilioni 12 za EPA kwa kutumia nyaraka zilizosainiwa na watumishi wa kampuni moja maarufu ya Dar es Salaam (jina tunalo) wakidaiwa kuwa wakurugenzi wa kampuni hiyo kabla ya kufahamika kwamba hawakuwa wakurugenzi halali kisheria. Kagoda, ambayo ilitumia nyaraka za kughushi, ilichotewa mabilioni hayo ya fedha kabla haijasajiliwa na katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Hadi sasa hakuna taarifa rasmi zinazoonyesha watu waliorejesha fedha za EPA kwa jina la Kagoda pamoja na kuwapo taarifa za uhakika kuhusiana na wafanyabiashara wazito waliorejesha fedha hizo kwa nyakati tofauti kabla ya muda uliowekwa kwisha Oktoba 31, 2008. Nyaraka zilizotumiwa na Afritainer kuchota mabilioni ya fedha za EPA mwaka 2000 zinaonyesha kwamba kampuni hiyo imetumia namba za simu 2861371 na 2861372 ambazo pia ndizo zimetumiwa na Kagoda katika kuchota fedha za EPA mwaka 2005. Namba hizo zinaonekana katika nyaraka za kampuni nyingine yenye uhusiano na wamiliki wa Afritainer. Nyaraka kutoka Wakala wa Usajili wa Makampuni na Leseni (BRELA) zinaonyesha kwamba Tabu Omari Masula na Barati A. Goda, walidaiwa kuingizwa kuwa wakurugenzi wa kampuni hiyo Mei 15, 2000 kinyume cha sheria. Barua ya BRELA ya Februarin 18, 2002, miaka miwili baada ya Tabu na Barati kuchota fedha za EPA, ilieleza kwamba wakurugenzi hao hawakuwa halali kutokana na kutokuwa na hisa katika kampuni ya Afritainer. Kwa mujibu wa barua hiyo kwenda kwa kampuni ya mawakili ya M.A.Imail, Tabu na Barati walikiuka kifungu cha 50 cha hati ya usajili ya kampuni hiyo kinachomlazimu mkurugenzi kuwa na hisa katika kampuni kwanza ili aweze kuwa na maamuzi. Waraka wa Afritainer uliowasilishwa BRELA Mei 15, 2000, ulieleza kwamba wakurugenzi pekee na waazilishi wa Afritainer ni Bahram Abdurasul Chakaar na Gulam Abdurasul Chakaar, wamejiuzulu ukurugenzi na kuwaachia Tabu na Barat. Hata hivyo, BRELA katika barua ya Februari 18, 2002 iliyoandikwa na Msajili Msaidizi wa wakala huo, L. Kimaro, ilieleza wazi kwamba hadi wakati huo ubadilishaji wa wakurugenzi haukuwa umeidhinishwa kutokana na kutokufuata masharti ya usajili. Tabu anatajwa kufanya kazi katika kampuni moja ya jijini Dar es Salaam yenye ofisi zake eneo la viwanda barabara ya Nyerere na Upanga. Kwa mujibu wa habari ambazo Raia Mwema imezipata fedha hizo kiasi cha Sh. Bilioni 13 zilichukuliwa Agosti 2000 kabla ya uchaguzi wa pili wa vyama vingi ambao Benjamin Mkapa aligombea tena urais. Waidhinishaji wakuu wa mikataba ya uchukuaji wa fedha hizo walikuwa ni mawakili maarufu wa kampuni ya uwakili ya Law Associates chini ya mkuu wake Dk. Ringo Tenga. Dk. Tenga sasa ni mwanasheria wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Nyaraka za uchukuaji wa fedha hizo mwaka 2000 zinaonyesha kwamba benki ya Akiba Bank ilitumika kupitishia fedha hizo kutokea BoT. Haikuweza kufahamika mara moja kama vyombo vya dola vimefanikisha kupata nyaraka husika, pamoja na kuwapo taarifa kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilikwishachunguza nyaraka hizo ikiwa ni pamoja na kuwahoji watumishi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kuhusiana na na matumizi ya namba za simu 2861372 na fax zilizotumiwa na kampuni ya Afritainer na Kagoda Agricultural. Kwa sasa wafuatiliaji wa sakata la EPA wanasubiri wahusika wa kampuni ya Kagoda Agricultural Limited iliyochota Sh bilioni 40 kufikishwa mahakamani baada ya kufikishwa kwa watuhumiwa wengine 20 hadi sasa. Tayari inafahamika kwamba kati ya shilingi bilioni 90 zilizoibwa katika akaunti ya EPA, sehemu kubwa ilichukuliwa na kampuni ya Kagoda Agricultural Limited ambayo hadi sasa wahusika wake hawajaguswa pamoja na kujitokeza kwa vigogo wawili kurejesha fedha zilizoibwa na kampuni hiyo. Vyanzo vya uhakika vinaeleza kwamba sehemu kubwa ya Shilingi bilioni 90 zilizothibitika kuchukuliwa kihalifu zilichukuliwa na makundi mawili tu, kundi la kwanza likiwa chini ya Jeetu Patel na lingine likiwa chini ya usimamizi wa vigogo wawili waliotumia kampuni ya Kagoda. Imefahamika kwamba kwa sasa kuna hekaheka kubwa za kutaka kuzuia kushitakiwa kwa wahusika wa Kagoda, lakini vyanzo vya ndani ya serikali vimeeleza kwamba kwa sasa serikali haitabiriki na lolote linaweza kutokea wakati wowote kabla ya mwisho wa mwaka. Kumekuwa na utata kuhusiana na ilipo na umiliki wa Kagoda Agricultural Limited ambayo imethibitika kujichotea kiasi cha Dola za Marekani 30,732,658.82 (zaidi ya Sh Bilioni 40/-) kutoka akaunti ya EPA na hakuna anayeweza kubainisha hasa zilipo ofisi na wahusika wa kampuni hiyo tata. Kumbukumbu za BRELA zinaonyesha kwamba ofisi zake zipo Kipawa Industrial Area Plot namba 87, Temeke, Dar es Salaam lakini eneo hilo lina makampuni tofauti jirani lakini namba iliyotajwa haionekani na badala yake eneo lenye ofisi na kampuni viwanja vyenye namba 77, 86 na 88 katika eneo hilo la viwanda. Katika ukaguzi wake wa awali wa mkaguzi wa nje Samuel Sithole kutoka kampuni ya Kimataifa ya Deloitte & Touche yenye makao yake Afrika Kusini alionya kuhusu matendo ya kihalifu ndani ya Kagoda kabla ya kuandikiwa barua na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji kwamba fedha hizo zilienda katika mambo "nyeti" ya kiusalama. Hata hivyo siku nne baada ya kuandika barua hiyo, Meghji alifuta barua hiyo akielezea kupotoshwa na aliyekua Gavana, Dk. Daudi Ballali, uamuzi ambao ulimgharimu kwa kiasi kikubwa mwanamama huyo makini ambaye alijikuta akiachwa nje ya Baraza la Mawaziri. Jamani tunaliwa na wenye meno !! Masikini Tanzania !! Je huyu ndiye Tenga wa Richmond AU ?

Source RAIA MWEMA

No comments:

Post a Comment